1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yalaani shambulizi la Israel dhidi ya Wapalestina Gaza

Amina Mjahid
1 Machi 2024

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema amekasirishwa na tukio la kuufyatulia risasi umati wa Wapalestina waliokuwa wamekusanyika kwenye kituo cha kutoa msaada mjini Gaza na kuwaua zaidi ya watu 100.

https://p.dw.com/p/4d439
Ufaransa| Rais Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alaani tukio la wanajeshi wa Israel kuwashambulia wapalestina waliokuwa wanapokea msaada Gaza Picha: Gonzalo Fuentes/AFP/Getty Images

Rais huyo wa Ufaransa alisema kile kilichomsikitisha ni kuona namna raia walivyolengwa na wanajeshi wa Israel.

Macron alilaani tukio hilo akitoa wito wa kuwepo ukweli, haki na kuheshimiwa sheria ya kimataifa, huku akisema ni muhimu kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa haraka.

Akizungumza katika redio moja ya Ufaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo, Stephane Sejourné, alisema nchi yake iko tayari kuunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa kufanya uchunguzi huru wa tukio hilo la siku ya Alhamis (Februari 29).

Kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas mjini Gaza, wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi Wapalestina waliokuwa wakipokea msaada wa chakula na kusababisha vifo vya watu 112 na wengine zaidi ya 750 kujeruhiwa.

Gaza | Hopsitali ya Al-Aqsa Martyrs
Wapalestina waliojeruhiwa kufuatia shambulio la Israel wakimbizwa hospitalini GazaPicha: Ali Hamad/APA Images via ZUMA Pres/picture alliance

Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza

Rais Joe Biden wa Marekani alisema tukio hilo lingelitatiza hatua za kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika mzozo huo wa takribani miezi mitano.

Msemaji wa serikali yake, Mathew Miller, alisema bado Marekani ilikuwa inachunguza kujua ni kipi hasa kilichotokea.     

Uturuki yasema Israel imefanya uhalifu mwengine dhidi ya ubinaadamu

Uturuki nayo iliishutumu Israel kwa kufanya uhalifu mwingine dhidi ya ubinaadamu kwa kuwalenga kwa makusudi Wapalestina wasio kuwa na hatia kwa lengo la kuwaangamiza.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: TUR Presidency/Murat Cetinmuhurdar/Handout/Anadolu via picture alliance

Kupitia kwa msemaji wake, Stephan Dujarric, Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia aliyalaani mauaji hayo akisisitiza kuwa watu wa Gaza wanahitaji msaada wa haraka, wakiwemo wale walio upande uliozingirwa wa kaskazini, ambako Umoja huo bado haujafanikiwa kupeleka misaada ya kibinaadamu.

Umoja wa Ulaya, China, Qatar, Saudi Arabia, Austaralia na mataifa mengine yalilaani tukio hilo na kusema ni uonevu kwa watu wa Palestina, huku wakitoa mwito wa makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa haraka ili kuwalinda watu wa Gaza wanaoendelea kuteseka.

Haniyeh: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini pia kuendeleza mapigano

Kolombia yatangaza kusitisha kununua silaha Israel

Rais Gustavo Petro wa Kolombia aliishutumu Israel kufanya mauaji ya halaiki mjini Gaza na kutangaza kusimamisha kwa muda ununuzi wa silaha za Israel.

Rais Gustavo Petro wa Kolombia.
Rais Gustavo Petro wa Kolombia.Picha: Ken Ishii/AP Photo/picture alliance

Israel ni moja ya mataifa yanayouza silaha zake kwa taifa hilo la Amerika ya Kusini, ambazo hutumika katika mapambano yake ya muda mrefu na wanamgambo pamoja na magenge ya wahalifu wanaoendesha biashara ya madawa ya kulevya.

Rais Petro alisema ni lazima dunia ikomeshe matendo ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, dhidi ya Wapalestina.

Israel yakanusha kuhusika na mauaji

Lakini Israel ilikanusha kuhusika na kutoa lawama ya moja kwa moja kwa umati wa watu uliokuwa unapokea msaada huo.

Mauaji ya Gaza
Picha ya angani ikionesha jinsi wanajeshi wa Israel walivyowalenga na kuwashambulia Wapalestina waliokuwa wakifuatilia malori ya misaada mjini Gaza.Picha: Anadolu/picture alliance

Badala yake, Israel ilisema waathiriwa waliuawa katika mkanyagano na msukumano, wakati walipoyazingira malori 38 ya msaada.

Jeshi la nchi hiyo lilikwenda mbali zaidi kwa kusema huenda madereva wa malori hayo waliwakanyaga Wapalestina waliokuwa wanasubiri msaada huo.

Licha ya tamko hilo, mmoja ya maafisa wa Israel baadaye alikiri kuwa wanajeshi wao waliwamiminia risasi Wapalestina kwa sababu walidhani ni kitisho kwa usalama wao.

Wapalestina zaidi ya 30,000 wameshauwawa tangu vita hivyo vianze mnamo Oktoba 7, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

AP/AFP/Reuters