1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaukaribisha mwaka mpya 2019

Sekione Kitojo
1 Januari 2019

Fashifashi, matamasha, huduma za  kiroho na  hotuba za  kisiasa  ndivyo vilivyoukaribisha  mwaka  mpya 2019, wakati watu waliokuwa  wakipata burudani  duniani  kote wakiuaga  mwaka 2018 jana Jumatatu.

https://p.dw.com/p/3Ar2a
USA New York Neujahrsfeier am Times Square
Picha: Reuters/D. Ornitz

Mwaka  2018 ni  mwaka  uliojaa  changamoto  kwa  taasisi  nyingi  duniani, ikiwa  ni  pamoja na  nyanja  ya  siasa, biashara , ushirika  na  dini. Mvua  kubwa haikuwazuwia makundi  ya  watu  kuujaza uwanja  maarufu  wa  Times Square  kwa  ajili  ya sherehe  hizo  za  kila  mwaka  mjini  New York, zikiambatana  na muziki  wa nyota  kadhaa  wa  muziki.

USA Neujahrsfeier in Las Vegas
Fashifashi ziliangaza angani mjini Las Vegas nchini Marekani katika kuukaribisha mwaka mpya 2019Picha: Getty Images/E. Miller

Christina Aguilera  aliwaburudisha  maelfu  ya  watu, akijitokeza  na  vazi  lake jeupe, huku  wapenda  muziki  wakisherehekea  katika  mvua. Watu  walilipa hadi dola 10  kupata  vazi  la  pancho ambalo ni  la  plastiki  ili  kuweza kujikinga  na  mvua  hiyo.

Mjini  Rio de Janeiro  nchini  Brazil  zaidi  ya  watu  milioni  2 walisherehekea kuingia  kwa  mwaka  mpya  katika  ufukwe  wa  Copacabana. Fashifashi zilizorushwa  kwa  muda  wa  dakika  14 ziliingiza Brazil  katika   mwaka  2019 masaa machache  tu  kabla  ya  mwanasiasa  wa  siasa  kali  za  mrengo  wa kulia  Jair Bolsonaro  kuapishwa   kuwa  rais  wa  nchi  hiyo. Wabrazil  wengi walikuwa  barabarani  kwenda  katika  mji  mkuu  wa Brasilia  usiku  wa  jana kuangalia  kuapishwa  kwa kapteni  huyo  wa  zamani  wa  jeshi  la  Brazil atakapoapishwa  mchana  wa  Jumanne.

Japan Tokyo Auto fährt in Fußgänger
Polisi wakiwa karibu na gari iliyowagonga watu katika mkesha wa mwaka mpya mjini TokyoPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Mjini  London  Waingereza  na  familia  zao  waliukaribisha  mwaka  mpya kwa  kengele  cha  saa  kubwa  ya  Big Ben, licha  ya  kuwa  saa  hiyo maarufu  duniani imezimwa  kwa  zaidi  ya  mwaka  sasa  kutokana  na  mradi wa  kuikarabati. Bunge  lilitangaza  wiki  iliyopita  kwamba  kengele  kubwa  ya saa  hiyo itatoa  sauti  kuadhimisha  kuingia  kwa  mwaka  mpya  kwa  msaada wa mfumo  maalum  wa  kielektroniki  kutoa  nishati  kwa  nyundo  yake, ambayo  ina  uzito wa  kilo 200.

Maandamano ya sherehe

Mjini  Paris wakaazi  wa  mji  huo  walikusanyika  katika  eneo  la  uwanja  wa Champ-Elysee  kusherehekea  mkesha  wa  mwaka  mpya  chini  ya  ulinzi mkali. Waandamanaji wanaoipinga  serikali kutoka  katika  vuguvugu linalojulikana  kama   vizibao  vya  manjano wametoa  miito  katika  mitandao ya  kijamii , kufanya "sherehe  za  maandamano"  katika  mtaa  huo mashuhuri. 

Großbritanien | Silvester – London
Sherehe za mwaka mpya mjini London kuukaribisha mwaka 2019Picha: picture alliance / empics

Polisi  nchini  Ufaransa  iliweka  uzio  katika  eneo  hilo, huku wakifanya  upekuzi  wa  mifuko, kupiga  marufuku  pombe na  kuzuwia magari  kuingia  katika  eneo  hilo. Wizara  ya  mambo  ya  ndani  imesema siku  ya  Jumapili  kuwa  hatua  kali  za  usalama  zinahitajika  kwasababu  ya "kitisho  cha  juu  cha  ugaidi" na  wasi  wasi  juu  ya "maandamano ambayo hayakutangazwa."

Rais Emmanuel Macron  alitoa hotuba  yake  ya  kawaida  kwa  mwaka  mpya na  kueleza  kwa  ufupi  malengo  ya  mwaka  2019, baadhi  ya waandamanaji  wakikasirishwa  na  kodi  kubwa  pamoja  na  upendeleo wake kwa  biashara , waandamanaji  wanapanga  kuendelea  na  maandamano katika  wiki  zijazo.

Mjini  Berlin  mamia  kwa  maelfu ya  watu walisherehekea  kuanza  mwaka 2019 katika  eneo  maarufu  mjini  berlin  la  lango  la  Brandenburg.

Deutschland | Silvester – Berlin
Sherehe za mwaka mpya katika uwanja wa eneo la lango la Brandenburg mjini BerlinPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Utumwa mamboleo wakemewa

Sherehe  za  kila  mwaka  za  mwaka  mpya  zilifanyika  huku  kukiwa  na ulinzi  mkali , ambapo  kiasi  ya  maafisa  wa  polisi  1,300 waliwekwa  katika kila eneo  la  mji  huo  mkuu  wa  Ujerumani  na  watu  walipigwa  marufuku kubeba  fashifashi, chupa  ama  mifuko  mikubwa  na  kuingia  navyo katika eneo  hilo la  sherehe.

Ilipofika  usiku  wa  manane , polisi  ya  mjini  Berlin iliripoti matukio machache  ikilinganishwa  na   mwaka  uliopita.

Vatikan Papst Franziskus beim Angelus-Gebet am Neujahrsmorgen
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis akiongoza misa katika kanisa la mtakatifu Petro mjini Vatican kukaribisha mwaka 2019Picha: Getty Images/AFP/A. Pizzoli

Kiongozi  wa  kanisa  Katoliki  ameueleza  mwaka  uliopita  kuwa  mwaka  wa matatizo  katika  wakati  wake  akiwa  madarakani kwa  kuendesha  misa  na sala  mbele  ya sanamu  kubwa  la  mchanga  la  mtu  wa  asili  katika  eneo hilo  la  makao  makuu  ya  kanisa. Katika  misa  hiyo  aliyoendesha , Francis alilalamikia  juu  ya  vile  watu  wengi  waliishi  katika  mwaka  2018 katika ukingo wa  utu, kutokuwa  na  nyumba ama  kulazimika  kuingia  katika  aina ya utumwa  wa  kimamboleo.

Akiongozana  na  mkuu  wake  wa  kutoa sadaka , Francis  alikwenda  nje  ya uwanja  wa  Mtakatifu  Petro , ambako  alisalimiana  na  mahujaji  na  kusali kabla  mbele  ya  sanamu  hilo  la  mtu  wa  asili , lililochongwa  kutokana  na mchana wa  tani 720.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Zainab Aziz