1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati

31 Agosti 2009

Utawala wa Rais Obama na pengine rais mwenyewe binafsi inaripotiwa kwamba atazindua duru mpya ya mazungumzo ya amani kati ya Mamlaka ya Wapalestina na Israel wakati wa kikao kijacho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/JLbq
**CLARIFIES THAT PRESIDENT OBAMA IS SPEAKING** U.S. President Barack Obama addresses an audience at the Cairo University in Cairo, Egypt Thursday, June 4, 2009. Speaking in the ancient seat of Islamic learning and culture, and quoting from the Quran for emphasis, President Obama called for a "new beginning between the United States and Muslims", and said together, they could confront violent extremism across the globe and advance the timeless search for peace in the Middle East. "This cycle of suspicion and discord must end," Obama said in the widely anticipated speech in one of the world's largest Muslim countries, an address designed to reframe relations after the terrorist attacks of Sept. 11, 2001, and the U.S.-led war in Iraq.(AP Photo/Ben Curtis)
Rais wa Marekani Barack Obama.Picha: AP

Kikao hicho kinatarajiwa kuanza hapo tarehe 15 mwezi wa Septemba mjini New York Marekani.

Je duru hiyo mpya ya mazungumzo inaweza kupiga hatua kwa kuondokana na kikwazo cha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Hadi hivi sasa vyombo vya habari vimekuwa vikizingatia zaidi mvutano unaoendelea wa utawala huo wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu juu ya kuendelea kwa mradi wa ujenzi wa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.Habari za juhudi kuu zinazofanyika kwa matarajio ya kufikiwa kwa amani kati ya Israel na Wapalestina hazikuzingatiwa sana.

Masuala hayo yanahusiana; Kuendelea kwa Israel kujenga makaazi yasio halali katika Ukingo wa Magharibi kunamega sana ardhi ya taifa lolote lile la baadae la Palestina.Hata mtetezi mkuu wa amani Mahmoud Abbas ambaye ni Rais wa Mamlaka ya Mpito ya Wapalestina na kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO amesema hawezi kushiriki katika mazungumzo ya kuamua hatima ya taifa hilo venginevyo Israel inasitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Msimamo huo wa Abbas umekuwa ukiungwa mkono kikamilifu na viongozi wengine wa Kipalestina na vyama kikiwemo kile cha Hamas.(Hata hivyo Abbas amesema huenda akakutana na Netanyahu wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa bila ya hata kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi hayo ya walowezi wa Kiyahudi.Lakini hakuainisha iwapo mkutano huo utakuwa chini ya maudhui ya mazungumzo ya amani).

Kuendelezwa kwa mradi wa ujenzi wa makaazi ya walowezi na Israel daima imekuwa sababu kuu yenye kudhoofisha imani ambayo Wapalestina wangelikuwa nayo kwa nia njema ya serikali ya Israel.

Ujenzi huo wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi pia unakiuka mpango wa ramani ya amani ulioandaliwa na Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush na washirika wake katika kundi la kimataifa la pande nne juu ya amani ya Mashariki ya Kati.

Baadhi ya wachambuzi wa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Waarabu wanaona kuendelea kuurefusha zaidi mvutano huo wa ujenzi wa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi itakuwa ni kupoteza wakati na nguvu ya mtaji wa kisiasa wa Obama wa ndani ya nchi na kimataifa.

Wachambuzi hao wanasema makubaliano yoyote yale ya mwisho ya amani yatajumuisha mipaka kati ya Israel na taifa la baadae la Palestina.

Mara mipaka hiyo itakapokuwa imechorwa suala la iwapo na wapi Israel inaweza kujenga nyumba mpya kwa wananchi wake litakuwa limebadilika mara moja.Baada ya kuwekwa kwa mipaka hiyo Israel itaweza kujenga kwa uhuru ndani ya mipaka yake kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Wapalestina wanatakiwa kupatiwa hakikisho la kutosha kwamba duru mpya ya mazungumzo haitoishia vibaya na bila ya mafanikio kama mazungumzo ya Annapolis ambayo Rais Bush aliyazindua kwa shangwe hapo mwaka 2007.

Bush aliahidi atafanikisha mazungumzo ya mwisho ya amani kabla ya kumalizika muda wake madarakani.Hilo kamwe halikutokea na wala usitishaji wa ujenzi wa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi kama inavyotakiwa na mpango wa ramani ya amani na kuyakinishwa huko Annapolis nchini Marekani.

Mazungumzo hayo ya Annapolis yalikuwa ya mwisho katika mfululizo mrefu ulioanzia na Mkutano wa Amani wa Madrid hapo mwaka 1991 ambapo viongozi wa Wapalestina waliahidiwa kwamba amani ya mwisho itafikiwa kwa haraka.

Wapalestina wanahitaji hakikisho zaidi kuonyesha kwamba Marekani iko makini zaidi leo hii kuliko ilivyokuwa wakati wa Annapolis.

Mwandishi: Mohamed Dhaman

Mhariri: Grace Kabogo