1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ehud Olmert akabiliwa na wakati mgumu

2 Mei 2007

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert kisiasa anakabiliwa na hali ya sintofahamu baada ya mwanachama mkuu katika chama chake kumtaka ajiuzulu kufuatia ripoti ya vita vya mwaka jana vya Lebanon.

https://p.dw.com/p/CHEz
Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert
Waziri mkuu wa Israel Ehud OlmertPicha: AP

Avigdor Yitzhak ni mmoja kati wanachama wenye uwezo mkubwa katika chama cha Kadima kinacho ongozwa na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.

Yitzhak amesema kuwa chama hicho kimepoteza uaminifu wake dhidi ya waziri mkuu Ehud Olmert ikiwa pia ni pamoja na wananchi wa Israel.

Bibi Tzippi Livni, waziri wa mambo ya nje anatarajiwa kukutana na waziri mkuu Ehud Olmert ili kumkabidhi sharti la mwisho.

Duru za waandishi wa habari zinadokeza kuwa bibi Livni huenda akamtaka waziri mkuu Ehud Olmert ajiuzulu la sivyo yeye atawaongoza wanachama wa chama cha Kadima katika kumuasi bwana Olmert.

Matamshi ya awali bibi Zippi Livni yaliashiria kuwa anataka bwana Ehud Olmert ajiuzulu kufuatia ripoti ya tume iliyoundwa na serikali kumlaumu waziri huyo mkuu kwa kushindwa vibaya katika vita vya Lebanon.

Kwa mujibu wa radio ya taifa na ile ya kijeshi nchini Israel, waziri wa ulinzi Amir Peretz anatafakari juu ya kujiuzulu kufikia kesho jumatano kwa kuwa lawama hizo pia zinamkabili.

Akilihutubia baraza la mawaziri kwa mara ya kwanza tangu ripoti hiyo itoke waziri mkuu Ehud Olmert alikiri kushindwa kwa serikali yake katika vita hivyo vya Lebanon na idadi kubwa ya mawaziri wake wamekiri kuwa wote wanahusika na kushindwa huko.

Bwana Olmert amesema ni wazi kuwa ripoti hiyo inaashiria kushindwa vibaya kwa serikali yake na hivyo kushindwa huko kunamlekea yeye zaidi kama kiongozi wa serikali hiyo lakini amewataka wale wote wanaokimbilia kujinufaisha kisiasa kutokana na ripoti hiyo wasifanye pupa.

O ton……..napendekeza kuwa wale wanaotaka kuitumia ripoti hiyo kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa waende tararibu.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert alikata kauli ya kuanzisha kampeni dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah mwezi julai mwaka jana.

Wazairi mkuu bwana Olmert analaumiwa na tume ya Winograd kwamba mapendekezo yake ya kuingia vitani kwa ajili ya kuwaokowa wanajeshi wawili wa Israel waliotekwa na kundi la Hezbollah na wakati huo huo kutaka kulimaliza kabisa kundi hilo la Hezbollah yalikuwa ndoto ambayo haingekuwa rahisi kuafikiwa katika siku 34 za vita.

Mkuu wa jeshi la Israel Dan Halutz alijiuzulu mapema mwaka huu na tangu ripotia hiyo itolewe siku ya jumatatu waziri mmoja katika serikali ya mseto kutoka chama cha Labour alijiuzulu hapo jana kabla ya vuguvugu hilo kusambaa hadi ndani ya chma cha bwana Ehud Olmert cha Kadima.

Wanasiasa wawili ambao wako mstari wa mbele kuchukua nafasi ya bwana Olmert ni bibi Zippi Livni kachero wa zamani wa Mossad na kaimu waziri mkuu Shimon Peres ammbe amewahi kuhudumu mara mbili katika wadhfa wa uwaziri mkuu.

Waziri mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu wa chama cha mlengo wa kulia cha Likud anatazamiwa pia kuchaguliwa kwa mujibu wa kura ya maoni iwapo serikali ya Ehud Olmert itaangushwa.