1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EILAT: Watu watatu wauwawa kwenye shambulio la bomu

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWc

Watu wasiopungua watatu wameuwawa kufuatia shambulio la bomu la mtu wa kujitolea mhanga maisha kwenye karakana ya kuoka mikate katika mji wa mapumziko wa Eilat kusini mwa Israel.

Shambulio hilo ni la kwanza kufanywa nchini Israel katika kipindi cha miezi tisa na ni la kwanza kuwahi kufanywa dhidi ya mji wa kusini wa Eilat.

Msemaji wa chama tawala cha Hamas nchini Palestina amelisifu shambulio hilo akilitaja kuwa jibu kwa sera za Israel.

Makundi matatu ya kipalestina yamejigamba kuhusika na shambulio hilo yakiwemo Islamic Jihad, Al Aqsa Martyrs´ Brigades na kundi linalojiita Army of Believers yaani Jeshi la Waumini.

Msemaji wa kundi la Islamic Jihad amesema mshambuliaji aliyetekeleza shambulio hilo aliingia kusini mwa Israel akitokea Jordan baada ya miezi saba ya matayarisho.