1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England haimo Euro 2008

Ramadhan Ali22 Novemba 2007

Orodha ya timu 16 zitakazoania kombe la Ulaya la mataifa kuanzia Juni 7 mwakani nchini Uswisi na Austria, sasa imekamilika,lakini bila ya Uingereza,”mama wa kabumbu”.

https://p.dw.com/p/CQMY
David BeckhamPicha: AP

Uingereza jana ilizabwa mabao 3-2 na Croatia wakati ikihitaji sare tu uwanjani Wemley, kujiunga na dola kuu za kabumbu za Ulaya-Itali,Ufaransa,Ujerumani,Holland na Spain.

Kocha wa England, Steve McClaren amejitwika dhamana ya pigo hilo,lakini anadai hatajiuzulu.

Russia jana ilijiunga na Sweden,Uturuki na Ureno kuwa timu za mwisho zilizotia tiketi zao mfukoni kwa kombe la ulaya la mataifa-la pili kwa ukali na msisimko baada ya kombe la dunia la FIFA.

Russia imekuwa timu ya 16 na ya mwisho kukata tiketi yake baada ya kikosi cha kocha Guus Hiddink, kuikuka kama chura Uingereza, kufuatia ushindi wao wa bao 1:0 dhidi ya Andorra.

Croatia ilikwisha tia kibindoni tiketi yake ya finali za kombe la ulaya; na mpambano wa jana na timu iliovumbua dimba-England ulikuwa ada tu.

Rais wa chama cha mpira cha Uingereza (FA) BRIAN BARWICK alikataa kusema iwapo kocha McClaren, atapigwa shoka katika kikao kilichoanza asubuhi ya leo cha FA.Matokeo ya jana maana yake, England imemaliza 3 katika kundi lake na akina David Beckham na Steve Gerrad, hawana lao jambo pale firimbi ikilia Juni 7 mwakani, kuziita timu 16 bora za Ulaya uwanjani.Kocha wa Croatia hakukosea aliposema, “ Uingereza imevumbua dimba,lakini hailitawali.”

Ujerumani,ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Jamhuri ya Czech katika kundi lake baada ya kumudu suluhu tu 0:0 na Wales.

Timu nyengine zinazokamilisha listi ya kombe lijalo la Ulaya, ni mabingwa Ugiriki,mabingwa wa dunia-Itali,Ureno,makamo-bingwa,Romania,wenyeji Uswisi na Austria.

Nje ya kombe la Ulaya ,Brazil jana ilitoka nyuma na kuipiku Uruguay kwa mabao 2:1 katika kinyan’ganyiro cha kanda ya Amerika kusini kuania tiketi za kombe la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.Paraguay, ikaizaba Chile 3:0 na kuparamia kileleni mwa kanda hiyo.Ecuador iiliikumta Peru mabao 5-1.