1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Wapiganaji wa Tigray walaumiwa kwa ubakaji

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
16 Februari 2022

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amenesty International limesema wapiganaji wa Tigray waliwaua raia kwa kudhamiria na pia waliwabaka wanawake na wasichana wadogo kwenye miji miwili ya jimbo la Amhara.

https://p.dw.com/p/477Ck
Hongkong Schließung Büro Amnesty International
Picha: TYRONE SIU/REUTERS

Uhalifu huo ulitendeka wakati wa vita vya miezi 14 kati ya majeshi ya serikali kuu ya Ethiopia na majeshi ya waasi wa jimbo la Tigray, TPLF. Kwa mujibu wa taarifa ya asasi ya haki za binadamu ya Amnesty International, baadhi ya wasichana waliobakwa walikuwa na umri wa miaka 14.

Nusu ya wanawake waliotendewa ukatili huo wamesema walibakwa na watu wengi kwa mpigo. Dada mmoja amesema mama yake pia alifanyiwa uhalifu na wapiganaji wa TPLF. Ushahidi unaonyesha kuwa majeshi ya Tigray yalitenda uhalifu wa kivita dhidi ya ubinadamu kwenye maeneo ya jimbo la Amhara kuanzia mwezi wa Julai na kuendelea mnamo mwaka uliopita. Wanawake walibakwa na raia waliuliwa kiholela.

Mama kutoka jimbo la Tigray anayesema alibakwa na kundi la wapiganaji wa Amhara
Mama kutoka jimbo la Tigray anayesema alibakwa na kundi la wapiganaji wa AmharaPicha: Nariman El-Mofty/AP/picture allianc

Naibu Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki Sarah Jackson amesema hospitali pia zilishambuliwa. Wakaazi wa mji wa Kobo wamesema raia ambao hawakuwa na silaha walipigwa risasi na waasi wa TPLF ili kulipiza kisasi baada ya kukabiliwa ya majeshi ya serikali kuu yaliyojibu vikali mashambulio ya waasi hao.

Soma zaidi:Kamati ya Nobel yasema Abiy ana jukumu maalumu katika mzozo wa Tigray 

Mpaka sasa waasi wa TPLF hawajajibu madai hayo, hata hivyo wamelilaumu shirika la Amnesty International juu ya ripoti yake iliyotolewa hapo awali kuhusu ukatili uliofanyika kwenye mji wa Nifas Mewcha na wamesema kuwa watafanya uchunguzi wao wenyewe.

Mwanamke wa Tigray aliyebakwa na ambaye amekimbilia mashariki mwa Sudan.
Mwanamke wa Tigray aliyebakwa na ambaye amekimbilia mashariki mwa Sudan.Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture allianc

Wakimbizi kadhaa kutoka jamii tofauti za Watigray wameliambiashirika la habari la  AP kwamba walishuhudia bila msaada wowote wakati wanawake walipochukuliwa na wapiganaji wa Amhara au wa Eritrea na kubakwa. Pamekuwapo na taarifa juu ya mauji ya raia na ubakaji wakati wa vita vya nchini Ethiopia.

Maalfu ya watu waliuliwa na maalfu wengine walikumbwa na baa la njaa. Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Umoja wa Mataifa na tume ya haki za binadamu ya Ethiopia uliochapishwa mwezi Novemba mwaka uliopita umebainisha kwamba pande zote mbili ambazo ni majeshi ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Tigray walitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Chanzo: AFP