1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yafanya mashambulizi kwa siku ya nne Tigray

John Juma
22 Oktoba 2021

Mashambulizi ya ndege za jeshi la Ethiopia Ijumaa yameilazimisha ndege ya misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa kutotua katika mji wa jimbo linalokumbwa na machafuko la Tigray, ni kulingana na watoa misaada.

https://p.dw.com/p/422ox
Äthiopien | Luftangriff auf der äthiopische Armee auf Mekelle
Picha: Million Haileselassie/DW

Mashambulizi ya viikosi vya Ethiopia katika jimbo la Tigray yameingia siku ya nne mfululizo tangu serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuanza wimbi jipya la mashambulizi. Msemaji wa serikali ya Ethiopia pia amethibitisha kwamba maafisa walijua kuhusu ndege hiyo ya Umoja wa Mataifa. 

Matukio ya Ijumaa yanaonekana kuthibitisha ongezeko la vitendo vya vitisho ambavyo maafisa wa Ethiopia wametumia dhidi ya watoaji misaada ya kiutu, mnamo wakati machafuko hayo ya Tigray ambayo yamedumu kwa mwaka mmoja sasa yakiendelea kuchacha.

Soma: Mashambulizi ya anga yautikisa mji mkuu wa Tigray

Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu ameliambia shirika la habari la Associated Press (AP) kwamba maafisa wao walijua kwamba ndege ya Umoja wa Mataifa ilikuwa katika eneo hilo lakini ndege hiyo pamoja na zile za kijeshi za Ethiopia zilikuwa sehemu tofauti tena kwa wakati tofauti. Haikubainika mara moja ndege za kivita za Ethiopia zilikuwa karibu kiasi gani na ndege hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Kulingana na Legesse, mashambulizi ya angani ya jeshi la Ethiopia katika mji wa Mekele, yalilenga kituo cha zamani cha mazoezi ambacho kwa sasa kinatumiwa na vikosi vya Tigray kama kituo cha mikakati au mipango ya kivita.

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Ethiopia imekuwa ikiyashutumu baadhi ya makundi ya kutoa misaada kwamba yanaunga mkono vikosi vya Tigray.
Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Ethiopia imekuwa ikiyashutumu baadhi ya makundi ya kutoa misaada kwamba yanaunga mkono vikosi vya Tigray.Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Msemaji wa jeshi hakutoa jibu mara moja alipoulizwa kuhusu tukio hilo la ndege ya Umoja wa Mataifa ambayo ilipanga kutua katika kambi kuu ya operesheni za misaada ya kiutu iliyoko Mekele jimbo la Tigray.

Soma: Shinikizo laongezeka dhidi ya serikali ya Ethiopia kuhusu jimbo la Tigray

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Ethiopia imekuwa ikiyashutumu baadhi ya makundi ya kutoa misaada kwamba yanaunga mkono vikosi vya Tigray. Mwezi uliopita serikali ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kuwafukuza maafisa saba wa Umoja wa Mataifa ikiwatuhumu bila kutoa ushahidi kwa kupotosha kuhusu viwango vya juu vya machafuko katika jimbo la Tigray.

Maafisa pia wamelazimisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kufanyiwa upekuzi, huku wakitekeleza kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa kizuizi dhidi ya misaada ya kiutu katika jimbo ambalo shirika la habari la AP limeripoti kwamba watu milioni sita wameanza kukabiliwa na njaa na kukenuliwa meno na mauti. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mzozo wa Tigray kuwa mbaya zaidi.

Wakaazi wa Mekele wamethibitisha mashambulizi ya hivi karibuni, mmoja akisema shambulizi moja lilifanywa karibu na chuo kikuu cha Mekele. Hakukuwa na tarifa ya moja kwa moja kuhusu maafa yoyote.

Machafuko ya Tigray yalianza mwaka uliopita pale Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoamuru operesheni dhidi ya kijeshi dhidi ya vikosi vilivyoasi vya Tigray.
Machafuko ya Tigray yalianza mwaka uliopita pale Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoamuru operesheni dhidi ya kijeshi dhidi ya vikosi vilivyoasi vya Tigray.Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Msemaji wa vikosi vya Tigray amekanusha madai kwamba kituo chao kilicholengwa mapema wiki hii kilikuwa kikitumiwa kuhusiana na mapigano.

Wafanyakazi wa afya pamoja na wakaazi wamesema watoto wasiopungua watatu wameuawa na zaidi ya watu kumi wamejeruhiwa.

Maelfu ya watu wameuawa tangu machafuko hayo yalipoanza Novemba mwaka jana kufuatia tofauti za kisiasa kati ya vikosi vya Tigray na utawala wa sasa wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Mnamo Alhamisi, serikali ilikiri kufanya shambulizi jingine dhidi ya kambi ya wapiganaji wa Tigray karibu na Mekele, lakini msemaji wa vikosi vya Tigray Getachew Reda alidai mfumo wao wa ulinzi wa angani ulizuia ndege kushambulia maeneo yaliyolengwa ndani ya mji.

Mawasiliano yamezuiwa katika jimbo la Tigray hivyo uhakiki huru wa madai yanayotolewa huwa mgumu.

(APE)