1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU katika mgogoro mzito na Urusi

Saumu Mwasimba
28 Machi 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wazidi kuumizwa kichwa na sakata la kushambuliwa kwa sumu jaasusi wa zamani wa Urusi Uingereza na matokeo ya kisa hicho,wanahisi ni kuvurumai la patashika

https://p.dw.com/p/2v7TR
Brüssel Nato-Hauptquartier
Picha: Getty Images/AFP/M. Wenger

Mada muhimu zilizowashughulisha wahariri leo ni chuki dhidi ya wageni barani ulaya,kisa cha kushambuliwa kwa sumu jasusi wa zamani wa Urusi katika ardhi ya Uingereza na mvutano ulioibuka kuhusu kisa hicho kati ya Uingereza,washirika wake dhidi ya Urusi, Sakata la kutumiwa kwa data za watumiaji wa Facebook.

Westfälischen Nachrichten

Visa vya chuki dhidi ya wageni vinavyoripotiwa katika shule kadhaa mjini Berlin vimeutamausha umma wa Ujerumani na kunyooshewa vidole moja kwa moja Kansela Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya ndani Seehofer katika suala zima la kuutazama uislamu. Kilichoibuka ni mjadala unaoashiria wazi kwamba utaratibu mzima wa ujumuishaji hauna tija. Mhariri huyo anaendelea kusema kwamba serikali inabidi iingilie kati kusaidia kifedha ili kuweka sawa huduma za kuwatunza watoto na pia elimu bora mashuleni, sambamba na kuweko mipango ya kutowatenga wageni katika mfumo pamoja na kuzuia uingiliaji wa kigeni katika vyama vya misikitini. Kwa maneno mengine ni kusema kuwa katika hili Ujerumani inajukumu la kuwajibika.

Volksstimme Linasema

Wayahudi  Ufarsansa wanabidi kuhofia uhai na maisha yao. Hilo limethibitika wazi baada ya kuuwawa kikatili mwanamke ajuza wa miaka 85 Mireille Knoll mjini Paris. Msingi wa mauaji hayo ni chuki iliyoongezeka ya muda mrefu dhidi ya wageni katika nchi hiyo jirani, ambayo imeshindwa kukabiliana nayo.Katika nchi hiyo ni wazi kwamba jamii ya waisilamu kwa sehemu kubwa imetengwa.Na hapana shaka yoyote kwamba hali hiyo imesababisha hasira ambazo zinaelekezwa kwa wayahudi nchini humo wanaoonekana kama wawakilishi wa Israel kama nembo ya maadui wakubwa wa Uislamu.Kijamii na kisiasa chuki dhidi ya wayahudi umeonekana kuwa mtindo barani Ulaya. Mhariri huyo anasema kwamba nchini Ujerumani kutokana na historia ya mauaji dhidi ya wayahudi ya Holocoust jamii hiyo imekuwa ikiwekewa ulinzi mkubwa.Lakini ubaguzi sio siri tena kwamba unaongezeka na kinachotia khofu zaidi ni kuonekana chuki za waziwazi dhidi ya wayahudi hasa mashuleni.

 «Sächsische Zeitung»Limeandika

Msimamo wa Ujerumani wa kuichukulia hatua Urusi inaonesha kwamba hata nayo pia haijaangalia mbali. Kinachojitokeza kwenye hili ni kwamba haijayaangalia maslahi yake,na kwamba mgogoro huu unaweza kusambaa na kuibua mvutano mkubwa zaidi ambao hautokuwa rahisi kuuzima.Kwa maana hiyo nini hasa kitakachofuatia? Je balozi za Urusi zifungwe? au ni kusema Urusi itawekewa  vikwazo zaidi vya kiuchumi?Au tuseme kwamba michuano ya soka ya kombe la dunia nchini Urusi itasusiwa? Kwa hakika zote hizo zitakuwa ni hatua za kuharibiana. Na mwisho wa yote hakuna yoyote atakayekuwa mshindi.

Kuhusu kutumiwa data za watumiaji wa Facebook na makampuni.«Hannoversche Allgemeine Zeitung»

Ni kitu gani  hasa kilichopo zaidi ya Facebook? Hapa ndipo palipo na fursa pekee na muda wa kukikomesha kile ambacho kinaonekana ni kundi la matajiri wachache wanaotengeneza mabilioni ya fedha  kwa kutumia data za watumiaji  wa Facebook dunia nzima. Mitandao mikubwa iwe ni Facebook,Google au Amazon ni lazima idhibitiwe kwa ushindani. Ulimwengu unabidi kufahamu kwamba tangu mwanzoni mwa miaka ya enzi za viwanda hii ni mitandao ambayo ilijijengea hali ya ukiritimba ya kulidhibiti soko la mtandao.Na kwa maana hiyo mitandao hii kwa sheria zake haiwezi kujali kulinda data za watu bali zitajishughulisha zaidi na sheria za kudhibiti ushindani.

 

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo