1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2016: Kivumbi cha nusu fainali

4 Julai 2016

Hatua ya Nusu fainali ya dimba la Euro 2016 inaanza Jutamano wiki hii, wakati Ureno itamenyana na Wales, nayo Ujerumani ikishuka dimbani na wenyeji Ufaransa siku ya Alhamisi

https://p.dw.com/p/1JIup
UEFA EURO 2016 Viertelfinale Polen vs Portugal Portugal gewinnt Quaresma
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mchuano wa Ureno na Wales mjini Lyon unaonekana kuwa vita vikali kati ya wacnezaji wenza wa Real Madrid Cristiano Ronaldo na Gareth Bale, lakini wachezaji hao wawili wenye thamani kubwa kabisa ulimwenguni hawaoni hivyo.

Hakuna kati yeyote kati ya nyota hao aliyefunga bao katika hatua ya mtoano ya dimba hili kabla ya kutinga nusu fainali. Ronaldo alifunga mabao mawili katika sare ya 3-3 na Hungary katika hatua ya makundi wakati Bale alifunga mara tatu katika hatua ya makundi.

Bale anasema utakuwa mchuano kati ya Ureno na Wales. Kocha wa Ureno Fernando Santos anasema „mpambano kati ya Ronaldo na Bale pekee hautaamua matokeo ya nusu fainali hiyo. Chris Coleman ni mkufunzi wa Wales "tunawafahamu, na tunajua kitisho chao. Ningeweza kuwapa mafunzo mabeki wangu kwa mwezi mmoja, ya kumkaba Ronaldo, lakini anaweza bado kuwa na nafasi ya kufanya maajabu yasiyoweza kuzuiwa. Lakini nasi pia tuna Gareth Bale kikosini hivyo itakuwa nusu kwa nusu.Tutafanya kazi yetu tu iliyotufikisha hapa kwa mara ya kwanza natusisahau hilo. Huo ndo mtindo wetu na tuko imara".

Frankreich Euro 2016 Wales - Belgien Sam Vokes Tor Jubel
Wales itamtegemea Gareth BalePicha: picture alliance/AP Photo/P. D. Josek

Wales watakosa huduma za Aaron Ramsey na Ben Davies ambao wamefungiwa mechi moja.

Ureno walifika nusu fainali bila kushinda mechi yoyote katika dakika 90, maana walitoka sare mara tatu katika hatua ya makundi, wakaipiga Croatia moja bila katka muda wa ziada na Poland kupitia penalti.

Ujerumani dhidi ya Ufaransa

Furaha inayoongezeka ya taifa zima baada ya Ufaransa kufuzu katika nusu fainali ya imeongeza motisha kwa Ujerumani wakati wanajiandaa kuwakabili siku ya Alhamisi. Hayo ni kwa mujibu wa kocha wa Die Mannschaft Joachim Loew.

Wajerumani, ambao watastahili kuifanyia mabidiliko timu yao kutokana na majeruhi Sami Khedira na Mario Gomez na kufungiwa mchuano mmoja beki Mats Hummels, wanajiandaa kuvaana na timu ambayo imejawa na matumaini. Timu ya Loew ilitinga nusu fainali baada ya mchuano ulioamuliwa na penalti dhidi ya Italia "Ulikuwa mchuano mgumu sana. hadi mkwaju wa mwisho wa penalti. nimewahi kushudia hilo mara moja au mbili hapo kabla, kwa mfano mwaka wa 2006 dhidi ya Argentina. Mchuano huo ulikuwa wa ufundi wa hali ya juu kwa timu zote. tuliudhibiti mpira na tukawazuia wataliano ambao wanapenda sana kushambulia kupitia katikati mwa uwanja".

UEFA EURO 2016 Deutschland vs. Italien
Joachim Loew alipata ushindi dhidi ya mwenzake wa Italia Antonio ContePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kocha huyo wa Ujerumani anasema baada ya kuibwaga Italia, sasa ni wakati wa kulenga taji lenyewe "bila shaka, ukiwa katika nusu fainali, lengo lako kuu ni fainali. Sasa tunastahili kuhakikisha kuwa wachezaji wetu wana muda wa kutosha kujiongeza nguvu. Unahisi uchovu baada ya mchuano kama huo. Sasa tunastahili kuhakikisha tunakuwa tayari katika siku mbili au tatu. lakini sasa tunataka zaidi

Ufaransa kwa upande wake itajaribu kuwapiku mabingwa hao wa dunia katika mchuano wa ushindani kwa mara ya kwanza tangu Kombe la Dunia la 1958, ijapokuwa waliwashinda katika mchuano wa kirafiki Novemba mwaka jana. Ufaransa itatafuta kulipiza kisasi vichapo vya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka wa 1982 na 1986 na hivi karibuni kichapo cha robo fainali cha 1-0 katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Kocha wa Les Bleus Didier Deschamps anasema matokeo ya jana hayataiwekea mbinyo Ujerumani na akawaonya wachezaji wake kuwa makini na ubora wa die mannschaft "Mchuano dhidi ya Ujerumani hautakuwa sawa na ulivyokuwa wa Iceland, kwa sababu Ujerumani ni timu yenye ubora wa kiufundi, hata kipa na mabeki, hivyo kwa jumla wanaudhibiti mpira. Tutazoea sio tu kwa nguvu zao, lakini pia kuhusu tutakachoweza kufanya. Kufikia sasa, isipokuwa Uswisi, tumepambana na wapinzani wanaojikinga zaidi. Dhidi ya Ujerumani itakuwa tofauti, lakini tutawalazimu kujikinga.

Wenyeji Ufaransa walikuwa kifua mbele 4-0 katika kipindi cha kwanza kabla ya mechi kukamilika katika ushindi wa mabao matano kwa mawili. Lakini kichapo hicho hakikuathiri fahari ya Iceland ambayo ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo. Mashabiki wa Iceland na wachezaji walisherehekea kwa pamoja kwa muda mrefu hata baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, na kikosi kizima kikapigwa picha mbele ya mashabiki wake. Kocha mwenza Lars Lagerback, ambaye sasa anamkabidhi majukumu ya ukufunzi

UEFA EURO 2016 Public Viewing in Reykjavík Frankreich vs Island Fans
Ufaransa wanalenga kutwaa taji katika ardhi ya nyumbaniPicha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Heimir Hallgrimsson baada ya miaka minne na nusu, amewapongeza vijana wake kwa kujitolea kuiwakilisha nchi yao kwa dhati "Uungaji mkono tuliopata kutoka kila mahali, nimekuwa Iceland na katika michuano na kila kitu hivyo umekuwa mzuri sana. Kuwaona mashabiki wote wakija hapa kutushangilia katika dimba hili na tulichosikia kutoka nyumbani, msisimko wote umekuwa wa kufurahisha.

Iceland wanaondoka Ufaransa walishindwa mara moja tu, lakini walitoka sare na Ureno na Hungary na kushinda dhidi ya Austria na England.

Mkataba wa kuzuia uhuni katika kandanda

Kwingineko, Urusi ni nchi 14 zilizosaini mkataba kati ya Baraza la Ulaya na Shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA unaolenga kuzuia marudio ya vurugu za mashabiki ambazo zilishuhudiwa katika dimba la Euro 2016.

UEFA imesema mkataba huo utajumuisha kubadilishana habari za kijasusi kati ya polisi ili kuzionya nchi zinazoandaa michuano kuhusu watu wanaoweza kuzusha ghasia.

Dimba la Euro linalochezwa nchini Ufaransa limeshuhudia kurejea kwa uhuni katika kandanda ambao haujashuhudiwa kwa kiasi kikubwa katika mashindano ya karibuni ya kimataifa.

Vurugu mbaya zaidi zilitokea mjini Marseille kabla na baada ya mchuano kati ya England na Urusi. Ufaransa, Bulgaria, Georgia, Ugiriki, Lithuania, Moldova, Monaco, Montenegro, Uholanzi, Ureno, Urusi, Uswisi, Macedonia na Ukraine ndizo nchi zilizosaini.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga