1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2020: Italia yauwa ndoto za England Wembley

12 Julai 2021

Baada ya kipindi cha karibu mwezi mmoja, mabao 145 ikiwa ni idadi kubwa zaidi ambayo tumewahi kushuhudia katika mashindano ya Ulaya, tamasha la euro 2020 limefikia tamati kwa Italia, kutwaa ubingwa

https://p.dw.com/p/3wLYQ
EURO2020 I Italien - England
Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Hadithi ya ukombozi wa kandanda la Italia imekamilika. Subira yenye uchungu ya nusu karne kwa England kushinda taji kubwa inaendelea. Na ni kwa sababu ya mikwaju ya penalti. Italia wameshinda Kombe la Ulaya – Euro 2020 kwa mara ya pili baada ya kuwafunga England 3 -2 kwa mikwaju ya penati jana usiku. Mechi ilimalizika 1-1 baada ya muda wa ziada dimbani Wembley, ambalo lilikuwa limefurika mashabiki 60,000 karibia wote wa england waliokuwa wamejiandaa kusheherehekea ubingwa wa kombe lao la kwanza la kimataifa tangu Kombe la Dunia la 1966.

Halikuja nyumbani. Badala yake, waItaliano waliharibu sherehe zao. Kocha Gareth Southgate ameihimiza England kutumia maumivu ya kupoteza fainali hiyo na kuangalia katika mafanikio ya siku za usoni. Southgate amekubali lawama ya kichapo hicho. Marcaus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka wote walikosa peanlti zao.

EURO 2020 | Finale Italien vs England
Italia ilikuwa timu bora ya mashindanoPicha: Laurence Griffiths/REUTERS

Vijana wa England walianza kwa kasi kupitia bao la dakika ya pili lake Luke Shaw lakini Italia ikaonyesha umahiri wake na kusawazisha kupitia Leonardo Bonucci katika kipindi cha pili.

Ilipofika mikwaju ya penati, Southgate alicheza karata zake kwa kuwaingiza uwanjani dakika za mwisho Rashford na Sancho hasa kwa sababu ya uwezo wao wa kupiga penati. Hatua hiyo iligonga ukuta. Southgate amesema anapaswa kulaumiwa kwa sababu yeye ndiye aliyewachagua wapiga penati.

Southgate amekiri kuwa vijana wake hawakuwa na utulivu kwenye mpira kitu ambacho kiliwaruhusu Waitaliano kurejesha udhibiti wao baada ya bao la Shaw. Amesema kipindi cha pili hawakuumiliki mpira vya kutosha.

Wakati Southgate akielezea udhaifu wao, Roberto Mancini alisema kutazama miaka mitatu ya kazi ngumu ikizaa matunda kwa ubingwa huu kumemtoa machozi. Italia ilipata kombe lao la mwisho la Ulaya 1968, na ni kazi murwa ya Mancini kukijenga upya kikosi baada ya kushindwa kufuzu katika Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi.

Kutoka kwa Gigi hadi Gigio

EURO 2020 | Finale Italien vs England
Donnarumma alipangua penati mbili ikiwemo ya SakaPicha: Paul Ellis/Getty Images/AFP

Kutoka kwa Gigi hadi Gigio, Italia bado ina kipa wa kutegemea mchumani. Miaka 15 baada ya Gianluigi Buffon kuisaidia Italia kushinda Kombe la Dunia katika mikwaju ya penati, Gianluigi Donnarumma alifanya hivyo hivyo dhidi ya England katika fainali ya Euro. Donnarumma aliokoa penati mbili za Saka na Sancho.

Donnarumma mwenye umri wa miaka 22 ambaye anahamia Paris Saint-Germain msimu ujao, ametawazwa mchezaji bora wa Euro 2020, na kuwa kipa wa kwanza katika historia ya mashindano hayo kutunukiwa tuzo hiyo.

Na baada ya ENGLAND kuzidiwa nguvu na Italia, Chama cha kandanda nchini England – FA kimetoa taarifa mapema leo kikilaani kauli za kibaguzi zilizofanywa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kichapo cha jana. Wachezaji wa England Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka, ambao wote ni weusi, walipoteza penati zao.

FA imesema itafanya kila liwezekanalo kusimama na wachezaji walioathirika na kuhimiza adhabu kali kuchukuliwa kwa yeyote anayehusika.

AFP, AP, Reuters, DPA