1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Facebook yatangaza hatua mpya kulinda data za watumiaji

Iddi Ssessanga
28 Machi 2018

Facebook imetangaza mabadiliko kadhaa kuwapa watumiaji udhibiti zaidi wa taarifa zao, baada ya kashfa kubwa ya data ilioigharimu zaidi ya dola bilioni 100. Marekebisho hayo yanafuatia ukosoaji mkubwa dhidi ya Facebook.

https://p.dw.com/p/2v94y
Facebook F8 Conference
Picha: Getty Images/J. Sullivan

Kampuni hiyo ilikumbana na malalamiko kutoka kona mbalimbali za dunia baada ya mfichuaji kubainisha Machi 17, kwamba data kutoka watumiaji milioni 50 zilichotwa isivyo sahihi kuwalenga wapigakura nchini Uingereza na Marekani katika chaguzi zilizokuwa na ushindani mkubwa.

"Wiki iliyopita imeonyesha ni kazi kiasi gani tunatakiwa kufanya kutekeleza sera zetu, na kuwasadia watu kuelewa namna Facebook inavyofanya kazi, na fursa za kuchaua walizonazo kuhusu taarifa zao,"  Erin Egan, makamu wa rais na mkuu anayehusika na faragha, na Ashlie Beringer, makamu wa rais na naibu wakili mkuu wa Facebook, waliandika katika chapisho la blogi.

"Hivyo, mbali na tangazo la Mark wiki iliyopita -- kuhusu kukabiliana na ukiukaji wa jukwaa la Facebook, kuimarisha sera zetu, na kuwarahisishia watu kuondoa uwezo wa App kutumia data zako-- tunachukuwa hatua za ziada katika wiki zijazo kuwapa watu udhibiti zaidi wa faragha zao."

Mark Zuckerberg Facebook
Mwanzilishi wa Facebook Marck Zuckerberg ameomba radhi kwa yaliotokea na kuahidi hatua za kulinda faragha za watumiaji.Picha: Getty Images/P. Marotta

Sheria ya ulinzi wa data EU njiani

Hatua hizo zinakuja kabla ya kupitishwa kwa sheria ya kihitoria kuhusu ulinzi wa data katika Umoja wa Ulaya mwezi Mei. Mtandao huo wa kijamii utaongeza menu ya njia za mkato za faragha, ambayo itawawezesha watumiaji duniani kote kupitia yale walioyashirikisha na kuyafuta, na pia vipengele vinavyowawezesha kupakuwa data zao na kuzihamishia kwenye huduma nyingine.

Hisa za Facebook zimeanguka kwa karibu asilimia 18 tangu Machi 17. Data za watumiaji zilichukuliwa isivyo halali na kampuni ya ushauri wa kisiasa ya Uingereza, Cambridge Analytica, ambayo ilipewa kazi na kampeni ya Donald Trump mwaka 2016.

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Mark Zuckerberg, ameomba radhi mara kwa mara na kununua kurasa nzima za matangazo katika magazeti ya Marekani na Uingereza, akiahidi kufanya kazi ya ziada kudhibiti upatikanaji wa data za watumiaji.

Wakati Facebook ilisema siku ya Jumatano kwamba mabadiliko iliokuwa ikiyatangaza yalikuwa katika maandalizi kwa muda sasa, ilisema matukio ya "siku kadhaa zilizopita yametilia mkazo umuhimu wake."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Josephat Charo