1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Familia za wapinzani zalengwa Misri

Lilian Mtono
19 Novemba 2019

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Righst Watch limeituhumu serikali ya Misri kwa kuwakamata watu wenye mahusiano na wapinzani, kufanya misako kwenye makaazi yao kuwahoji na kuwazuia kusafiri.

https://p.dw.com/p/3TIAh
Ägypten, Kairo: Sicherheitskräfte Symbolbild
Picha: picture-alliance/AP/A. Nabil

Kwenye ripoti hiyo ya Human Rights Watch iliyotolewa hii leo shirika hilo limerekodi visa 28 vya waandishi wa habari wa nchini humo, watumishi kwenye vyombo vya habari, wanasiasa pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu walioikosoa serikali na sasa wakiwa wanaishi nje ya nchi.

Visa ambavyo shirika hilo limevirekodi vilitokea kati ya mwaka 2016 na 2019.

Naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch wa eneo la Mashariki na Kaskazini mwa Afrika Joe Stork amenukuliwa akisema mamlaka za Misri zimekuwa zikiziadhibu familia za wapinzani wanaoishi ughaibuni, na kutoa mwito kwa serikali kusitisha mashambulizi na adhabu hizo dhidi yao.

Miongoni mwa visa ambavyo Huma Rights Watch imevirekodi ni vile vya vikosi vya usalama kuvamia makaazi ya familia 14 za wapinzani na katika visa vitano wanajeshi waliharibu mali za familia hizo bila hata ya kuonyesha waranti wa kupekua ama kumkamata mtu yoyote.

Serikali ya Misri pia iliwazuia kusafiri ama kuzikamata pasi za kusafiria za jamaa 20 za wapinzani wanane. Watu wengine 20 wenye mahusiano na wapinzani 11 walikamatwa na kushitakiwa.

Inhaftierte ägyptische Islamisten
Baadhi ya watu walikamatwa na kushitakiwa na serikali ya MisriPicha: picture-alliance/dpa/H. Khamis

Aidha zaidi ya wanaharakati na waandishi wa habari wanaoishi nje ya nchi wamesema wanajizuia kuikosoa serikali hadharani ama kujihusisha na shughuli nyingine za upinzani kwa sababu wanahofia kile kitakachozipata familia zao.

Mtangazaji wa kituo cha televisheni kilichopo Uturuki cha Al-Sharq Haytham Abu Khalil amelieleza shirika hilo kwamba Oktoba 2, mwaka huu vikosi vya wizara ya mambo ya ndani vilivamia makazi ya mama yake Fadia pamoja na dada yake Diana ambao wote wanaishi Alexandria, na kupekua makaazi ya dada yake kwa masaa kadhaa na kumuhoji kuhusu shughuli za ndugu zake huko ughaibuni.

Ägypten Präsident Abdel Fattah al-Sisi
Human Right Watch imeitaka Misri kusitisha vitendo hivyo vya uvamizi na kamatakamataPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya Abu Khalil kuchapisha picha kwenye kipindi chake cha televisheni ziliwaonyesha familia ya rais Abdel Fattah al-Sissi ikiwa kwenye shughuli mbalimbali.

Mohamed Ali aliyeko uhamishoni ambaye video yake aliyoichapisha kwenye mtandao wa Facebook kuhusu madai ya ufisadi wa serikali iliamsha maandamano makubwa dhidi ya serikali mwezi Septemba ameiambia Human Rights Watch kwamba siku kadhaa baada ya kutuma video hiyo mamlaka zilivamia kampuni yake ya ukandarasi mjini Cairo na kuwakamata angalau wafanyakazi 7 na kuwachilia watatu.

Septemba 19 mwanaharakati maarufu Wael Ghonim aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba vikosi vya usalama vilimkatama mdogo wake wa kiume Hazem baada ya Wael kuchapisha video kwenye Facebook za kuikosoa idara za usalama za serikali lakini pia walivamia chumba cha wazazi wake na kuchukua dola 28,000 pasi za kusafiri za familia na simu za mkononi.

Ujumbe ambao Misri inataka kuutuma uko wazi amesema Stork akimaanisha, ni onyo la wazi kwa wapinzani la kuacha kukosoa na hata kuzungumza hata kama unaishi ughaibuni kwa kuwa ni dhahiri familia yako itakuwa mashakani.