1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Federer anyakua taji la Gerry Webber Open

28 Juni 2017

Gwiji wa Uswizi katika mchezo wa Tennis Roger Federer alimgaragaza Mjerumani Alexander Zverev na kushinda taji lake la tisa la kipute cha Gerry Webber Open katika fainali iliyochezwa mjini Halle, hapa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2fW6Q
Deutschland ATP-Turnier Tennis in Halle - Federer vs. Zverev
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gentsch

Federer aliishinda mechi hiyo kwa urahisi kwa seti mbili za 6-1 6-3 katika mechi iliyodumu kwa dakika 53. Kwa ushindi huo Federer sasa alijinyakulia taji la 92 katika taaluma yake ya uchezaji ambapo amecheza fainali 140 "Kwa kweli nilikuwa najishuku kidogo, lazima nikiri hilo, kwasababu kupoteza raundi ya kwanza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15 ni jambo ambalo lilikuwa lazima linibabaishe na kweli lilinibabaisha. Kwa hiyo nina furaha na kufanya huko kupoteza seti ya kwanza kusahaulike na nijikumbushe kwmaba naweza kucheza vyema katika uwanja wa nyasi. Ushindi huu unanipa imani kubwa, kwa hiyo ninaufurahia sana hapa Halle. Najiskia vizuri kushinda hapa kwa mara nyengine tena kwasababu sijui kama nitapata fursa tena ya kushinda, kwa hiyo ni muhimu kufurahia."

Federer alikuwa anakitumia kipute hicho kama cha kupasha misuli moto ili ajiweke tayari kwa lile shindano kuu la Wimbledon huko Uingereza litakaloanza Julai 3. Anapigiwa upatu kuebuka mshindi katika shindano hilo na iwapo atamaliza kama bingwa, atakuwa ameweka rekodi kwa kushinda taji la nane na kuivuka ile rekodi ya mataji saba yaliyoshindwa na Pete Sampras ambaye kwa sasa wanaishikilia rekodi hiyo pamoja.

Kwa sasa Federer anaishikilia nafasi ya tatu katika wachezaji tennis walioshinda mataji mengi zaidi duniani, huku Ivan Lendl anayeorodheshwa wa pili akiwa amemzidi na mataji mawili tu.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE
Mhariri: Josephat Charo