1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Israil yawatia nguvuni viongozi wa Wapalestina

24 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByl

Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, amesema serikali yake haina uhusiano wowote na kundi la Fatah al-Islam linalopambana na majeshi nchini Lebanon.

Rais Mahmoud Abbas alisema hayo mjini Gaza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana.

Rais Abbas anayeongoza chama cha Fatah amesema serikali yake itawapelekea misaada ya kiutu wakimbizi wa kambi ya Nahr al-Barid ambako wanamgambo wamekuwa wakipamba na serikali.

Kwengineko Israil iliendelea na mashambulio ya ndege usiku kucha katika Ukanda wa Gaza na wakati huo huo ikawatia nguvuni wakuu thelathini na watatu wa chama cha Hamas katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Miongoni mwa waliokamatwa ni waziri wa elimu wa Palestina, Nasseredine al-Shaer, wabunge watatu na mameya wanne.

Msemaji wa kijeshi wa Israil amesema watu hao walikuwa wakiunga mkono mashambulio yanayotekelezwa dhidi ya Israil kutokea Gaza.

Wanamgambo wa kipalestina wamekataa wito wa Rais Mahmoud Abbas wasimamishe mashambulio ya makombora dhidi ya Israil, wakisema hawatasitisha mashambulizi yao mpaka Israil kwanza ikomeshe mashambulio yake.