1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Watu tisa wauwawa katika Ukanda wa Gaza

2 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD6u

Watu takriban tisa waliuwawa na wengine wasiopungua 100 wakajeruhiwa wakati wa mapigano kati ya vikosi vya usalama vinavyohasimiana katika Ukanda wa Gaza.

Machafuko hayo yameelezwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea ndani ya Palestina kufuatia miezi kadhaa ya wafanyakazi kutolipwa mishahara na kukwama kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa taifa. Waziri mkuu wa Palestina, Ismail Haniyeh, wa chama cha Hamas, amewatolea mwito wapalestina wasimamishe machafuko.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, wa chama cha Fatah, amesema hatoruhusu mapigano hayo yazidi na kuwa vita vya kikabila. Aidha Abbas ameapa kuwaadhibu wote waliohusika kusababisha machafuko hayo.

Mapigano yalianza wakati wanamgambo wa Hamas walipofyatua risasi kuyavunja maandamano ya watu waliokuwa wakidai malimbizi ya mishahara yao ambayo haijalipwa.

Wakilipiza kisasi, wafuasi wa chama cha Fatah walilivamia jengo la makao makuu ya Hamas na kulichoma moto mjini Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.