1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zazuka upya Misri

Admin.WagnerD16 Julai 2013

Mamia ya wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani nchini Misri Mohammed Mursi wamekabiliana na askari usalama na kiasi ya watu saba wameuawa na wengine zaidi ya 250 kujeruhiwa

https://p.dw.com/p/198Ha
Picha: Reuters

Hapo jana usiku mamia ya waandamanaji waliziba daraja lijulikanalo kama Oktoba 6 la kuvukia mto Nile katikati mwa mji mkuu Cairo na askari wa usalama waliwarushia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwafurusha kutoka daraja hilo na waandamanaji hao walijibu kwa kuwarushia maafisa hao mawe.

Waandamanaji hao wanataka kurejeshwa madarakani kwa Mursi na hizi ndizo ghasia za kwanza mjini Cairo tangu waandamanaji wengine kuuawa nje ya makao makuu ya jeshi Jumatatu iliyopita.

Jumuiya ya kimataifa yaingiwa wasiwasi

Saa chache kabla ya makabiliano hayo, afisa mkuu wa Marekani William Burns aliomba kuwe na mazungumzo badala ya ghasia na kulitaka jeshi la Misri kuepuka kuwakamata viongozi wa udugu wa kiislamu na wengine kutokana na kile alichokitaja kuchochewa kisiasa huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa kuhusiana na ukandamizaji wa udugu huo wa kiislamu.

Rais wa muda wa Misri Adly Mansour(Kulia)akutana na afisa wa Marekani William Burns
Rais wa muda wa Misri Adly Mansour(Kulia)akutana na afisa wa Marekani William BurnsPicha: Reuters

Mazungumzo yapewe nafasi

Burns amesema kinachopaswa kupewa kipaumbele ni mazungumzo na pande zote. Alikuwa akizungumza baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali mpya akiwemo waziri mkuu aliyeteuliwa na jeshi Hazem el Beblawi anayetarajiwa kulitangaza baraza jipya la mawaziri aidha leo au kesho.

Lakini udugu wa kiislamu umekataa kushiriki katika serikali ya mpito na wafuasi wake bado wanataka Mursi kurejeshwa madarakani.Msemaji wa udugu huo Farid Ismail ameishutumu Marekani kwa kuegemea upande mmoja katika mzozo unaoikumba Misri.

Marekani yashutumiwa katika mzozo wa Misri.waandamanaji waandamana kueleza ghadahabu yao
Marekani yashutumiwa katika mzozo wa Misri.waandamanaji waandamana kueleza ghadahabu yaoPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amethibitisha kuwa Burns hakukutana na maafisa wa udugu huo wa kiislamu.Na vuguvugu la Tamarod lililoandaa maandamano yaliyomng'oa madarakani Mursi pia limekataa kukutana naye kwasababu ya kile ilichosema kuwa Marekani haikuwaunga mkono watu wa Misri tokea mwanzo.

Ziara hiyo ya Burns inakuja huku maafisa wa serikali wakizidi kuwabinya wafuasi wa Mursi kwa kuzuia mali za viongozi 14 wa kiislamu huku nchi hiyo ikikumbwa na machafuko upya hasa katika eneo la Sinai na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban ki Moon akilaani kuandamwa kwa maafisa wa chama cha Udugu wa Kiislamu

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed