1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guaido azidi kumuwekea mbinyo Maduro kupitia misaada

Sekione Kitojo
21 Februari 2019

Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido amenakwenda katika mpaka na Colombia ili kuleta binafsi chakula na madawa  yaliyotolewa na Marekani akikaidi serikali inayoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3DnoW
Juan Guaido
Picha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

 Hali  hiyo inaongeza  wasi  wasi  juu  ya  makabiliano  makubwa  mwishoni  mwa  juma, kati  ya  rais Maduro na  Guaido.

Guaido, ambaye  ameweka  siku  ya  mwisho  ya  Jumamosi kuweka  kuingiza  misaada, amepanga  kuondoka   mapema  asubuhi leo Alhamis  katika  msafara  wa  mabasi  pamoja  na  wajumbe  wa bunge  la  taifa  linalodhibitiwa  na  upinzani, kulazimisha  makabiliano makubwa  na  rais Nicolas Maduro.

Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture-alliance/dpa/Z. Campos

Kwa  amri  ya  Maduro, jeshi limeongeza  ulinzi  mpakani  na  kuweka vizuwizi  katika daraja muhimu  la  mpakani  kuzuwia  biadhaa  hizo kuingia  katika  nchi  yake  kutoka Cucuta, Colombia, ambako  tani kadhaa  za  mahitaji  zimelundikana.

Licha ya  kwamba  hakuna  hakika  hasa  kile  ambacho  Guaido anataka  kufanya , amesema  ameorodhesha  mamia  kwa  maelfu ya  watu  wa  kujitolea  katika  siku  za  hivi  karibuni  kusaidia  kuleta biadhaa  hizo  pamoja  na  kuzigawa.

Jana  Jumatano , aliwahamasisha  madereva  wa  mabasi  kwenda katika  mpaka na  kubeba  bidhaa  hizo  za  msaada  kwa ajili  ya Wavenezuela wanaotaabika  kutokana  na  upungufu  wa  bidhaa hizo.

Blockierte Grenze zwischen Venezuela und Kolumbien
Daraja muhimu la mpakani kati ya Venezuela na Colombia ambako jeshi la Venezuela limeweka vizuwizi kuzuwia misaada ya Marekani kuingia nchi humoPicha: Getty Images/L. Robayo

Hatuogopi

"Hata  kama  watatuelekezea  bunduki , na  sisi  wote tumepokea vitisho, risasi  za  mipira  na  hata  risasi  za  moto , hatuogopi," Guaido  alisema,  akiwa  amesimama  juu  ya   lori  akizungukwa  na maelfu  ya  waungaji  wake  mkono.

"Tutasimama  mitaani  vifua  wazi , tukidai  uhuru kwa  Wavenezuela wote."

Shehena  ya  chakula  na  madawa  kwa  ajili  ya  watu waliokumbwa  na  mzozo  imekuwa  lengo  kuu  la  mvutano  wa madaraka  kati  ya  Maduro  na  Guaido.

Kiongozi  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  35 wa  bunge  la Venezuela  alijitangaza  kuwa  kaimu  rais Januari  23, na  tangu wakati  huo  amepata  uungwaji  mkono  wa  zaidi  ya  nchi  50.

Venezuela Krise - USA schicken weitere Hilfsgüter
Baadhi ya misaada kutoka Marekani ikiwa nchini ColombiaPicha: Reuters/E. Garrido

Anataka  kumuondoa  madarakani Maduro, kuunda  serikali  ya mpito  na  kufanya  uchaguzi. "Hii inaweza  kufikiwa  hivi  karibuni, kati  ya  miezi  sita  na  tisa, mra  pale upinzani  wa  Maduro utakapomalizika," Guaido ameiambia  televisheni  ya  Mexico Televisa.

Guaido  ambaye  anasema  watu  zaidi  ya  laki  tatu  huenda wakafariki  iwapo  misaada  hiyo  haitaingia,  amesema  ana  lengo la  kuwataka  mamilioni  ya  watu  wa  kujitolea  kuanza  kuingiza msaada  huo  nchini  humo  ifikapo  Jumamosi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusuf Saumu