1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres asema mashambulizi yanapaswa kusita Syria

Sekione Kitojo
26 Februari 2018

Mashambulizi mapya ya anga ya jeshi la Syria dhidi ya eneo la Ghouta Mashariki yamewauwa raia 10 wakati mataifa ya magharibi yanaongeza mbinyo kuyafanya makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya kusitisha mapigano yaanze kazi.

https://p.dw.com/p/2tMTI
Syrien Damaskus - Ost-Ghuta nach Luftangriffen
Picha: Reuters/B. Khabieh

Katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  Mataifa  Antonio Guterres  ametaka utekelezaji mara  moja  wa  azimio  linalotaka  kusitishwa  mapigano kwa  muda  wa  siku 30 nchini  Syria, wakati shambulio  jingine linaloshukiwa  kuwa  la silaha  za  sumu limesabisha  mtoto  mmoja kufariki katika eneo hilo.

UN Sicherheitsrat Abstimmung über Waffenruhe in Syrien
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa likipiga kuraPicha: picture alliance/ZUMAPRESS.com

"Ghouta mashariki haiwezi  kusubiri. Muda  umefika sasa  kusitisha mauaji  haya  ya  jahanamu hapa  duniani," Antonio Guterres alikiambia  kikao  cha  ufunguzi cha  37 cha  baraza  la  haki  za binadamu  la Umoja  wa  mataifa mjini  Geneva.

Azimio la baraza la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa lililopitishwa siku  ya  Jumamosi limeleta  matumaini kwamba  mashambulizi  ya wiki  nzima yaliyofanywa  na  jeshi  la  serikali  linaloungwa  mkono na  Urusi  ambayo  yamewauwa  raia  zaidi  ya 500 huenda yakafikia  mwisho.

Lakini  wakati  mashambulizi  makali  yalipungua kidogo mwishoni mwa  juma, ndege  za  kijeshi zimeendelea  na  mashambulizi  yao na  makombora  bado  yanarushwa  Ghouta mashariki. Miongoni mwa  wahanga  wa  hivi  karibuni  ni  watu  tisa  wa  familia  moja waliouwawa  pale  nyumba  yao  mjini  Douma, mji  mkuu  wa  eneo hilo, ilipoporomoka na  kuwaangukia.

Syrien Damaskus - Ost-Ghuta: Verwüstung nach Luftangriffen
Mashambulizi yalikuwa yakiendelea dhidi ya Ghouta masharikiPicha: picture-alliance/AA/Q. Noor

"Raia tisa kutoka  familia  moja  wameuwawa  katika  mashambulizi ya  majeshi  ya  serikali mjini  Douma, usiku wa  manane," Rami Abdel Rahman, mkuu  wa  shirika  la  kuangalia  haki  za  binadamu nchini  Syria  lenye  makao yake  makuu  nchini  Uingereza.

Baraza  la  taifa la usalama

Rais  wa Urusi  Vladimir  Putin wakati  huo  huo amejadili  hali katika eneo  la  mashariki  mwa  Ghouta nchini  Syria na baraza la  usalama la  taifa, shirika  la  habari  la  TASS limesema leo, likimnukuu msemaji  wa  serikali Dmitry Peskov. Peskov amesema kwamba baraza la usalama  la  Urusi limeeleza  wasiwasi  wake  juu ya vitendo  vya uchokozi vinavyofanywa  na  waasi  wa  Syria, kwa mujibu  wa  shirika  la  habari  la  TASS.

Jana  Jumapili, mtoto  mmoja  alifariki  na  wengine 13 walipata matatizo  ya  kupumua  na  kuonesha ishara za mara kwa  mara  za shambulio la gesi  ya  Klorini baada  ya  shambulio  la  majeshi  ya serikali  katika  mji  wa  Al-Shifuniyah, limesema  shirika  linaloangalia haki  za  binadamu  nchini  Syria. Urusi ilikanusha ripoti  hizo za mashambulizi  ya  silaha  za  sumu  kuwa ni  hadithi  zisizo  na maana. Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alisema:

Syrien Angriffe auf Ost-Ghuta
Mtoto na mtu mmoja wakionekana hospitali wakipatiwa huduma ya kupumua baada ya shambulio la gesi ya kloriniPicha: Reuters/B. Khabieh

"Baadhi  ya  maandiko ya  kupakana matope  tayari yameonekana katika  vyombo vya  habari yakisema sumu ya klorini ilitumika kama silaha  jana ama  asubuhi ya leo huko mashariki  mwa Ghouta. Ilifanyika  akinukuliwa  mtu mmoja ambaye  hakutajwa jina anayeishi Marekani. Nataka  kuwakumbusha kwamba  jana maafisa  wa  Urusi walishaonya  juu  ya  uchokozi  na bila  shaka  tayari tunaona katika majimbo ya kusini  mwa jamhuri  ya  Kiarabu  ya ,Syria  ambako Marekani , nina hakika, inajaribu kuweka hali ya Taifa tofauti na kuigawa Jamhuri wa  Kiarabu  ya  Syria."

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemweleza  rais  wa Uturuki  Recep Tayyip Erdogan  leo kuwa pendekezo  la  Umoja  wa mataifa  la  kusitisha  mapigano  nchini  Syria  linapaswa  kuhusisha nchi  nzima, ikiwa  ni  pamoja  na  jimbo  la  Afrin ambako  Uturuki inafanya  mashambulizi  dhidi ya  wanamgambo  wa  kikurdi.

Frankreich Treffen Macron und Erdogan
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki(kulia)Picha: picture alliance/abaca/Somer

Katika  mazungumzo  kwa  njia  ya  simu  baina  ya  viongozi  hao wawili, Macron alisema  usitisjaji  mapigano  wa  siku  30, unahusisha  ardhi  yote  ya  Syria, ikiwa  ni  pamoja  na  Afrin, na  ni lazima  yatekelezwe  kila  mahali  na  kila  mmoja  bila  kuchelewa, imesema  ofisi  ya  rais.

Mwandishi Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Josephat Charo