1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ayasihi mataifa kuendelea kuisaidia UNRWA

Angela Mdungu
28 Januari 2024

Wakati mapigano makali yakiripotiwa Gaza siku ya Jumapili, Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres ameyasihi mataifa wafadhili kuendelea kuliunga mkono shirika la umoja huo linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

https://p.dw.com/p/4blR0
New York |Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa UN, Antonio GuterresPicha: Manuel E./Xinhua News Agency/picture alliance

Guterres ametoa ombi hilo baada ya mataifa kadhaa likiwemo Ujerumani kusitisha ufadhili wao kutokana na tuhuma kuwa baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walihusika kwenye mashambulizi dhidi ya Israel Oktoba 7.

Katika  kauli yake Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, " Wakati ninaelewa wasiwasi wao - mimi mwenyewe nilishtushwa na tuhuma hizi - ninazisihi sana serikali ambazo zimesitisha michango yao, angalau, kuhakikisha shughuli za UNRWA zinaendelea".

Soma zaidi: Mataifa zaidi yasitisha ufadhili kwa shirika la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina

Umoja wa Mataifa tayari umesema unazichunguza tuhuma hizo za Israel zilizodai kuwa wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walihusika na mashambulizi yaliyopangwa na kundi la Hamas lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100 na kutekwa nyara kwa wengine 240.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la UNRWA limetoa ajira kwa karibu wafanyakazi 13,000 kwenye Ukanda wa Gaza. Guterres alithibitisha kuwa, kati ya wafanyakazi 12 walioorodheshwa katika tuhuma hizo, tisa wamefukuzwa kazi, mmoja ameuwawa na utambulisho wa wengine wawili unaendelea kuchunguzwa.

Watakaobainika kushiriki vitendo vya kigaidi kuchukuliwa hatua

Mkuu huyo wa UN ameapa kuwa mfanyakazi yeyote wa shirika hilo anayehusika kwenye vitendo vya kigaidi atawajibishwa ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashtaka ya jinai.

Wakati huohuo alisema kuwa maelfu ya wanawake wanaofanyakazi na UNRWA, wengi wao wakiwa katika mazingira magumu hawapaswi kuadhibiwa bali mahitaji makubwa ya watu waliokata tamaa wanaowahudumia hayana budi kutimizwa."

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini, ameyaomba pia mataifa yautafakari upya uamuzi wa kusitisha ufadhili kabla ya shirika hilo kulazimika kusitisha kutoa huduma zake.

Kamishna Mkuu wa Shirika la kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini
Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini Picha: Salvatore Di Nolfi/picture alliance/KEYSTONE

Tangu mzozo huo ulipoanza, zaidi ya wakaazi milioni 2.3 wa Gaza wamekuwa wakitegemea misaada inayotolewa na UNRWA

Majadiliano ya kuwaachilia mateka kuendelea Paris

Katika hatua nyingine, vyombo vya habari vya nchini Marekani vimearifu kuwa, mazungumzo yanayolenga kuwaachilia huru matekawengine wa Israel kutoka katika kundi la Hamas, yamepangwa kufanyika Jumapili mjini Paris.

Gazeti la The New York Times liliripoti kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA, William Burn atakutana na maafisa wa Israel, Misri na Qatar kwa mazungumzo katika mji huo mkuu wa Ufaransa. Nao maafisa wawili ambao waliomba wasitajwe majina yao waliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, inapendekezwa kuwa makubaliano yapitie awamu mbili.

Mateka Judith Tai Raanan  na Natalie Shoshana Raanan walipoachiliwa huru na Hamas Oktonba 20.
Baadhi ya mateka walioachiliwa huru na Hamas Oktoba 20,2023Picha: Government of Israel via REUTERS

Katika awamu ya kwanza, mapigano yanaweza kusitishwa ili kuruhusu wanawake waliosalia, wazee na mateka waliojeruhiwa waachiliwe na Hamas.

Katika siku 30 za kwanza za kusitishwa kwa mapigano, kisha Israel na Hamas wanaweza kufanyia kazi vipengele vya awamu ya pili ambapo wanajeshi na raia wa kiume wa Israel wanaweza kuachiliwa.

Mkataba unaopendekezwa unaripotiwa kuwa utawezesha misaada zaidi ya kibinaadamu kuingia Gaza