1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gwiji wa ndondi Muhammad Ali afariki dunia

4 Juni 2016

Bondia wa zamani Muhammad Ali, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo (04.06.2016) akiwa na umri wa miaka 74. Alikuwa amelazwa hospitali Phoenix, Arizona akiwa na matatizo ya kupumua wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/1J0OA
Muhammad Ali 2011
Picha: Getty Images/W. McNamee

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa familia yake, Ali amekufa baada ya kuugua ugonjwa wa Parkinson kwa miaka 32. Bob Gunnell, msemaji wa familia ya Ali amesema gwiji huyo wa zamani wa masumbwi duniani alikuwa amelazwa katika hospitali ya Phoenix katika jimbo la Arizona, akiwa na matatizo ya kupumua wiki hii.

Bingwa huyo mara tatu wa ndondi wa uzito wa juu, aliyejulikana pia kwa uanaharakati wa kijamii, aliwahi kulazwa hospitali mwaka 2014 baada ya kuugua homa ya mapafu, na kisha akalazwa tena mwaka uliopita kutokana na maambukizi katika njia ya kupitishia mkojo.

Ali alizaliwa kama "Cassius Clay" huko Louisville, Kentucky Janury 1942. Alianza mchezo wa masumbwi kama chipukizi alipokuwa na umri wa miaka 12. Mwaka 1964 alikuwa bingwa wa ndondi wakati alipomzidi nguvu Sonny Liston.

Muhammad Ali Bildergalerie Sonny Liston Knockout
Muhammad Ali alipomtwanga Sonny Liston, ukumbi wa St Dominic, Lewiston, Maine 1965Picha: Neil Leifer

Mabondia wenzake kama Sugar Ray Leonard wametoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Ali: "Maombi na baraka kwa shujaa wangu, rafiki yangu na bila shaka bingwa wa wakati wote@MuhammadAli!"

Ali alionekana hadharani mara ya mwisho Aprili katika tamasha la "Celebrity Fight Night" huko Arizona, shirika linalowasaidia wagonjwa wanaoishi na ugonjwa wa Parkinson, ambao Ali aligunduliwa nao miaka mitatu baada ya kustaafu kucheza ndondi mwaka 1981 na rekodi ya ushindi mara 56, na kushindwa mara tano.

Taaluma ya Ali ilitatizwa kwa zaidi ya miaka mitatu katika miaka ya 1960 wakati alipokataa kujiunga na jeshi la Marekani wakati wa vita vya Vietnam na akashitakiwa na kutiwa hatiani kwa kukwepa kusajiliwa jeshini. Mahakama ya juu kabisa ya Marekani ikaipundua hukumu hiyo. Baadaye Ali alishinda mataji mawili ya ndondi ya uzito wa juu kabla kustaafu mwaka 1981.

Mwandishi:Josephat Charo/ap/reuters

Mhariri:Yusra Buwayhid