1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadithi juu ya biashara ya watoto yashinda shindano

27 Agosti 2012

Washindi ni kundi la vijana kutoka Togo. Katika shindano hili, wasikilizaji wa Noa Bongo walipewa fursa ya kuelezea visa vyao binafsi na walielezea hadithi za kusisimua.

https://p.dw.com/p/15xDU
Bouloufèi Bèwèzima
Bouloufèi BèwèzimaPicha: Bouloufèi Bèwèzima

Bwana mmoja na mke wake wana watoto saba. Ingawa wanajitahidi sana, hawawezi kuwalea ipasavyo. Shangazi wa watoto anaahidi kuwachukua watoto wawili na kuwatunza. Lakini badala yake, anawapeleka Nigeria kufanya kazi na anawanyang'anya mshahara wao. Hii ni simulizi iliyotumwa na kijana Bouloufè Bèwèzima. Mwaka huu, yeye na kundi lake la vijana kutoka mji mkuu wa Togo, Lomé, wameibuka washindi katika shindano la uandishi la Noa Bongo.

Kwa bahati nzuri, kisa hiki kina mwisho mwema: Wale wavulana wawili wanafanikiwa kumtoroka shangazi yao na baada ya safari refu na hatimaye kurudi nyumbani kwa wazazi wao. Lakini katika maisha ya kila siku, visa vya namna hii mara nyingi huwa na mwisho mbaya. "Kila mwaka tunaona kwamba wapo watoto wanaokatisha masomo yao na kwenda Nigeria au katika nchi nyingine kufanya kazi kwa ajili ya kupata fedha za kununulia baisikeli, pikipiki ama cherehani," anaeleza mtunzi Bouloufè. "Wengi wao wanapotelea huko na hawarejei tena nyumbani."

Kisa binafsi kwa ajili ya mchezo wa redio

Loyce Maturu aliyeshiriki katika shindano la Noa Bongo
Loyce Maturu aliyeshiriki katika shindano la Noa BongoPicha: Andreas Keller

Kisa hiki, pamoja na simulizi nyingine zilizotumwa kama sehemu ya shindano la Noa Bongo, kimebuniwa kutokana na mambo yanayotokea kila siku na yanayoshuhudiwa na waandishi. Hadithi nyingi zilizotumwa ziligusia mada kama elimu, matatizo ya kifamilia, mimba zisizotarajiwa au haki za wanawake na watoto. Simulizi ya kundi la "Tsanga Jeunesse" kutoka kaskazini mwa Cameroon, kinamwelezea msichana mdogo aliyelazimishwa kuolewa na mwanaume mwenye umri mkubwa sana kuliko yeye. Simulizi hiyo imeshika nafasi ya pili katika shindano la Noa Bongo.

Nafasi ya tatu imenyakuliwa na kundi la "Zvandiri Youth Advocacy Team" kutoka Zimbabwe. Vijana wa kundi hilo wanajitolea kuwakinga watoto na vijana walioambukizwa virusi vya Ukimwi dhidi ya ubaguzi. Loyce Maturu, mmoja wa wanakikundi, anaeleza kwamba kuandika hadithi kwa ajili ya Noa Bongo kumewasaidia kutafakari juu ya kazi wanayoifanya. "Tukiwa shuleni na hata katika familia zetu tunashuhudia ubaguzi huu. Kwenye simulizi yetu tulitaka kuyagusia maeneo ambapo watoto na vijana wenye virusi vya ukimwi hukumbana na ubaguzi."

Mada zinazowagusa wote

Kundi la Zvandiri Youth Advocacy Team kutoka Zimbabwe
Kundi la Zvandiri Youth Advocacy Team kutoka ZimbabwePicha: Andreas Keller

Jambo linaloifanya Noa Bongo kukubalika na kupendwa kote barani Afrika, ni utayarifu wake wa kuzungumzia mada nzito. Simulizi zilizotumwa kwa ajili ya shindano zinaonyesha kwamba bado vipo visa vingi sana vinavyofaa kuelezewa. Hadithi 36 kutoka nchi 15 za Kiafrika zilishiriki katika shindano. Jopo la majaji watano kutoka idhaa za Kiafrika za DW lilikaa na kutathmini hadithi hizo.

Mmoja wa majaji hao alikuwa Zainab Mohmmed-Ahmed kutoka Idhaa ya Hausa. Yeye anaeleza kwamba ilikuwa vigumu kwake kuchagua mshindi kwani hadithi nyingi zilikuwa nzuri sana. Hata hivyo, simulizi iliyoshika nafasi ya kwanza ndiyo iliyompendeza zaidi. Kwa mtazamo wa Zainab, mada iliyozungumziwa ni ya muhimu kwani katika baadhi ya nchi za Kiafrika, biashara ya watoto ni jambo linalotokea. "Ni jambo lililopo zaidi miongoni mwa familia masikini zinazojaribu kujipatia maisha bora zaidi," anaeleza Zainab.

Warsha ya uigizaji kwa ajili ya washindi

Mwaka 2013 hadithi ya washindi kutoka Togo itafanyiwa mfululizo wa michezo ya redio kwa ajili ya Noa Bongo. Mbali na hayo, washindi pamoja na timu ya Noa Bongo wataandaa mchezo wa kuigiza kuhusu hadithi hiyo. Igizo hilo litaonyeshwa mjini Lomé. Ingawa mshindi ni mmoja tu, kundi la "Zvandiri Youth Advocacy Team" lililoshika nafasi ya tatu, nalo limeamua kuandaa mchezo wa kuigiza juu ya ubaguzi wa watu wenye Ukimwi. Igizo hilo litaonyeshwa kwa mara ya kwanza katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.

Mwandishi: Christine Bukania
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Khelef