1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za watoto hasa wakike zakiukwa zaidi nchini Morocco

16 Julai 2007

Licha ya taifa hilo kuwa na sheria inayopinga kuajiriwa watoto chini ya umri wa miaka 15 watoto hutumiwa zaidi kama vijakazi vya nyumbani nchini humo.

https://p.dw.com/p/CHkC

Mamia ya watoto hasa wakike wanatumiwa vibaya ikiwa ni pamoja na kuozwa kwa lazima kutokana na tamaduni za Morocco.

Sheria ya Morocco inapinga kuajiriwa kazi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 15 lakini hilo halijawazuia watu kuwatumia kama vijakazi vya nyumbani watoto hasa wakike walio na umri hata wa miaka 5.Watoto hao hufanyishwa kazi kwa muda mrefu na kupewa mateso ya kila aina ikiwa ni pamoja na kubakwa ikiwa kazi walioifanya hairidhishi.

Juu ya hilo watoto hao hawapewi nafasi ya kupata elemu,lishe bora na hata huduma ya matibabu.

Habiba Hamrouck mwenye umri wa miaka 22 amezungumzia juu ya madhila aliyoyapata akiwa mdogo wakati alipopelekwa kwenye familia moja mnamo mwaka 1990 anasema aliona kila aina ya mateso.Habiba anasema likuwa mtoto wa miaka 8 lakini alilazimishwa kufanya kila aina ya kazi ngumu.

Dadazake wadogo pia waliteseka kama alivyoteseka yeye kwani walilazimika kufanya kazi ya nyumbani kutokana kwasababu hali ya maisha nyumbani ilikuwa sio nzuri hata kidogo.Mamayao hakuwa na la kufanya ila kububujikwa na machozi kila dakika hasa akizingatia kwamba hakuwa na usemi mbele ya mumewe aliwalazimisha watoto kuwa vijakazi ili wapate fedha.

Habiba anasema alimchukia babake kutokana na uamuzi huo.

Hivi sasa akiwa ameolewa na umri wa miaka 22 na watoto wawili Habiba anafanya kila awezalo ili kunusuru maisha ya wanawe wawili wasitumbukie kwenye dimbwi la madhila aliyoyapata binasfi akiwa motto,

Hafida Hosman mwenye umri wa miaka 18 kisa chake sio tofauti na cha Habiba lakini yeye anasema alifanikiwa kuyakwepa madhila shukurani zimwendee jirani yake mmoja.

Akihadithia kisa chake anasema akiwa na umri wa miaka 14 mamake alimkabidhi kwa familia moja tajiri kabisa mjini Rabat na familia hiyo ilikuwa na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 16 basi kijana huyo alimtumia vibaya Hafida wakati wazazi wake hawapo lakini hakuweza kupeleka malalamiko yake mahala popote.

Na kwasababu kuzungumzia kuhusu ngono ni mwiko nchini Morocco basi wasichana wadogo wanapobakwa katika familia wanazozitumikia inakuwa vigumu kwao kuzungumzia matatizo yao.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na serikali kwa ushirikiano na shirika la kuwafadhili watoto la Umoja wa mataifa kiasi cha watoto wakike 22 elfu nchini Morocco wakiwa ni chini ya miaka 18 wanafanya kazi za nyumbani katika miji mikubwa kama Rabat na Casablanca.

Kiasi cha asilimia59 ya watoto hao ni wadogo chini ya miaka 15 kutoka familia masikini na zisizo na elimu.

Kutumiwa vibaya kwa watoto wakike sio jambo geni nchini humo shirika la kutetea haki za binadamu lilo na makao yake mjini New York Marekani lilitoa ripoti yake miaka miwili iliyopita na kulaani utesaji wa watoto majumbani huko Morocco.

Kati ya watoto waliohojiwa na shirika hilo wengi ilibainika kwa wengi wao wanafanya kazi kwa muda wa saa 14 hadi 18 kila siku kwa wiki nzima na mshahara ukiwa ni senti 4 hadi senti11.