1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo

Oumilkher Hamidou18 Novemba 2008

Baraza la usalama kujadili pendekezo la Ufaransa la kuzidishwa kwa muda wanajeshi wa Monuc

https://p.dw.com/p/Fx6r
Kambi ya wakimbizi huko GomaPicha: AP



Ufaransa imependekeza mswaada wa azimio mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa,kutaka idadi ya wanajeshi wa kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo iongezwe.



Mswaada huo wa azimio,unafuatia mwito uliowahi kutolewa na muakilishi wa Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,Alan Doss anaeongoza vikosi vya kulinda amani vya MONUC.


Mswaada huo unazungumzia juu ya kuongezwa kwa muda wanajeshi hadi 2785 wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo-MONUC pamoja na askari polisi wasiozidi 300.


Mswaada wa azimio ulioandaliwa na Ufaransa kwa ushirikiano pamoja na nchi kadhaa za magharibi,ikiwemo Ubeligiji,Uengereza na Marekani,unazungumzia pia umuhimu wa MONUC kuendesha shughuli zake kikamilifu,kama inavyotajwa katika kifungu nambari sabaa cha muongozo wa Umoja wa mataifa.Kifungu hicho kinashadidia haki ya MONUC kutumia nguvu ili kuwalinda raia.


Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa magharibi ambae hakutaka jina lake litajwe,mswaada huo wa azimio utajadiliwa hivi karibuni na baraza la usalama.


Wanajeshi 17 elfu wa kulinda amani ya Umoja wa mataifa MONUC,wamewekwa tangu mwaka 2001 katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,elfu tano kati yao katika mkoa wa Kivu ya kaskazini ambako mapigano yameripuka upya tangu Agosti mwaka huu,kati ya  waasi wanaoongozwa na Laurent Nkunda na jeshi la serikali.


Katika wakati ambapo waasi wanaonyesha kusonga mbele,wakipuuza makubaliano ya kuweka chini silaha katika eneo hilo la mashariki,rais Joseph Kabila amemteuwa mkuu wa vikosi vya wanamaji,  jenerali Didier Etumba Longomba kuongoza vikosi vya wanajeshi,badala ya Dieudonné Kayembe.


Mabadiliko hayo yametokea katika wakati ambapo jeshi la serikali limekua likilishwa hasara mtindo  mmoja tangu wiki kadhaa zilizopita  na waasi wa Laurent Nkunda wanaojikuta karibu na Goma.


Jumapili iliyopita waasi wa CNDP wanasemekana kuliteka eneo la Kanyabayonga na mji wa  Rwindi.Tume ya Umoja wa mataifa ya kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo Monuc imelaani mashambulio hayo na kusema yanakwenda na ahadi waasi walizompa muakilishi maalum wa umoja wa mataifa,Olusegun Obasanjo za kuheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha,waliyotangaza wenyewe mwishoni mwa mwezi uliopita.


CNDP wanahoji nyendo zao ni jibu kwa  mashambulio yanayofanywa na  jeshi la serikali.


Wakati huo huo ripoti za shirika la habari la Ufaransa zinazungumzia juu ya risasi zinazofyetuliwa tangu jana usiku katika maeneo ya Kayna na Kirumba karibu na Kanyabayonga,mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.


Hali ni shuwari kidogo  tangu asubuhi na haijulikani kama mapigano hayo ni ati ya wanajeshi wa serikali wenyewe kwa wenyewe au kati yao na wanamgambo wa Mai Mai,wanaoungwa mkono na serikali.