1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali mbaya ya hewa yauwa watu 160 Pakistan na Afghanistan

Daniel Gakuba
15 Januari 2020

Wafanyakazi wa uokozi nchini Pakistan wamepata miili ya watu 21 waliouawa na maporomoko ya theluji katika jimbo la Kashmir, na kuifanya idadi ya waliopoteza maisha nchini Pakistan na Afghanistan kufika 160.

https://p.dw.com/p/3WF3i
Kaschmir Lawine in Neelum Valley
Picha: Getty Images/AFP

Huduma za uokozi zinafanya kazi bila kupumzika kuwatafuta wahanga wengine ambao nyumba zao zimefunikwa na theluji ambayo ni nyingi zaidi kuanguka nchini Pakistan kwa muda wa karibu karne nzima. Eneo lililoathirika zaidi ni la Kashmir ya upande wa Pakistan, hususan bonde la Neelum ambako watu 21 wameuawa, na miili yao tayari imepatikana.

Waziri wa Pakistan anayehusika na huduma za dharura Ahmad Raza Qadri amesema tangu Jumapili iliyopita, hali mbaya ya hewa imesababisha vifo vya watu 76 katika jimbo la Kashmir upande ulio chini ya Mamlaka ya Pakistan, na wengine 45 wameuwa katika jimbo la Baluchistan kusini magharibi mwa nchini hiyo, na Punjab lililo upande wa mashariki.

Afghanistan Winter | Schnee in der Provinz Herat
Barabara katika mkoa wa Herat nchini Afghanistan hazipitikiPicha: DW/S. Tanha

Ahueni nchini Afghanistan

Nchini Afghanistan hali imeanza kuboreka leo, baada ya mafuriko na mvua kubwa kuwauwa watu 39 na kuziharibu nyumba za makaazi zipatazo 300 tangu Jumapili. Mkazi mmoja wa mjini Kabul, Wali Mohammad anasema kwa zaidi ya miongo mitatu walikuwa hawajashuhudia hali mbaya ya hewa kama hii.

''Mwaka huu unanikumbusha miaka 30 iliyopita ambapo mji wa Kabul ulikumbwa na baridi kali na theluji nyingi iliyoziba barabara. Nadhani baridi ya mwaka huu ni kama ya wakati ule'' amesema Mohammad na kuongeza kuwa katika majimbo ya Yakawlang, Bamyan na Kandahar watu wengi wamepoteza nyumba zao.

Afghanistan Winter | Schnee in Kabul | Armut
Wazee na watoto ndio walioathirika zaidiPicha: DW/G. Adeli

Wakaazi watumia mikono kuwanusuru wapendwa wao

Katika bonde na Neelum kazi kubwa ya uokozi inafanywa kwa ushirikiano wakaazi. Mmoja wa wakaazi hao, Lal Hussain Minhas ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu, kwamba ameweza kumvuta mke wa binamu yake, kutoka chini ya kifusi cha nyumba yake iliyobomolewa na poromoko la theluji.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema hali hii mbaya itaendelea kwa siku zijazo jimboni Kashmir. Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amewatembelea baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hospitali ya mji mkuu wa jimbo la Kashmir inayotawaliwa na Pakistan, Muzaffarabad.

Mkurugenzi mkuu wa idara ya hali ya hewa nchini Pakistan Mohammed Riaz amesema hali inayojiri ni ishara ya wazi kwamba mabadiliko ya tabianchi yameuathiri vikali ukanda ilipo Pakistan, na kuonya kuwa hali ya siku za usoni huenda ikawa mbaya zaidi.

dpae, ape