1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Libya

19 Septemba 2011

Wanajeshi wa utawala mpya wa Libya wameingia tena Bani Walid leo na wanaendelea kuuzingira mji wa Sirte, ngome za wafuasi wa kiongozi wa zamani .

https://p.dw.com/p/12c5f
Kiongozi wa baraza la mpito la Libya Mustafa Abdel DjalilPicha: dapd

Licha ya kusonga mbele wanajeshi wanaompinga Gaddafi katika uwanja wa mapigano, katika uwanja wa kisiasa hali haijulikani ikoje.Tangazo la kuundwa serikali mpya ya mpito lililokuwa litolewe jana usiku, limeahirishwa haijulikani mpaka lini, kwa sababu viongozi wapya wameshindwa kukubaliana kuhusu nani awemo na nani asiwemo katika serikali hiyo.

Baraza la mpito la taifa, linalotambuliwa na Umoja wa mataifa kama mwakilishi wa wananchi wa Libya, lilisema mapema mwezi huu linapanga kuiongoza nchi hiyo hadi uchaguzi wa baraza la kutunga katiba katika kipindi cha miezi minane ijayo, utakaofuatiwa na uchaguzi mkuu mwaka mmoja baadaye.

Kipindi cha miezi minane kingeanza lakini kwa mujibu wa watawala hao wapya wanaosema wanadhibiti asili mia 90 ya ardhi ya Libya, baada ya nchi nzima kukombolewa.

Libyen Rebellen in Bani Walid
Wanajeshi wa utawala mpya wa Libya wajiandaa kuingia Bani WalidPicha: dapd

Msemaji wa utawala wa Gaddafi, Mussa Ibrahim, amesema wanajeshi wao wameibuka na ushindi mnamo siku za hivi karibuni dhidi ya wale aliowaita "washirika wa NATO"."Tumefanikiwa kuwarejesha nyuma kutoka Bani Walid na Sirte," amesema kwa simu jana kupitia kituo cha televisheni cha Arrai chenye makao yake nchini Syria.

Mussa Ibrahim amesema pia kwamba wafuasi wao anaowaita "Mujahiddin" wamewateka nyara mamluki 17 huko Bani Walid, wengi wao anasema ni Wafaransa, Waingereza wawili, wawili wa kutoka Asia na mmoja wa kutoka Qatar. Serikali ya Uingereza mjini London imesema hii leo haiwezi kuthibitisha madai hayo.

Huko Bani Walid mapigano makali yameripotiwa hii leo kati ya vikosi vya baraza la mpito la taifa na wafuasi wa Muammar Gaddafi. Amesema hayo afisa mmoja wa utawala mpya katika eneo hilo, Abdallah Kenchil. Kwa maoni yake, wanategemea kuuteka mji huo mnamo siku mbili zijazo. Kwa maoni yake wapiganaji wa utawala wa zamani ni mamluki wa kutoka Chad, Niger na Togo. Amesema mazungumzo yanaendelezwa kuwaruhusu raia wapatao 50 elfu wauhame mji huo. Abdallah Kenchil amesema Saif el Islam, mmojawapo wa watoto wa Muammar Gaddafi ameonekana Bani Walid alikojificha pengine pia Muammar Gaddafi.

Sarkozy und Cameron in Libyen
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na waziri mkuu wa Uengereza David Cameron washangiriwa walipowasili LibyaPicha: picture alliance/abaca

Mjini Sirte, wanajeshi wa baraza la mpito la taifa wanajaribu zaidi kulinda njia kuu ili kuwaruhusu raia wauhame mji huo ili na wao wapate kujibu mashambulio ya mizinga ya waafuasi wa Gaddafi.

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema katika ripoti yake hii leo, imefanya hujuma za angani jana huko Sirte na Waddan, mojawapo ya miji mitatu ya mkoa wa Djofra, umbali wa kilomita 300 kusini mwa Misrata.

Kwa upande wa kiuchumi kampuni la mafuta la Ufaransa, Total, limesema hii leo linatazamiwa kuanza haraka shughuli zake nchini Libya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,afp

Mhariri:Josephat Charo