1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Thailand

Oumilkher Hamidou18 Mei 2010

Serikali yakataa pendekezo la wanachama 64 wa baraza la Senet kupatanisha mgogoro kati yake na "Mashati mekundu"

https://p.dw.com/p/NR5e
Waziri mkuu wa Thailand Abhisit VejjajivaPicha: AP

Serikali ya Thailand imeondowa uwezekano wa kuingilia kati baraza la Senet kupatanisha ugonvi unaotishia umoja wa nchi hiyo na ambao umeshagharimu maisha ya watu 67 tangu mwezi uliopita.

Pendekezo lililotolewa na wanachama 64 kati ya 150 wa baraza la Senet lilikubaliwa hapo awali na wanaharakati wa upande wa upinzani-Mashati mekundu,wanaodai waziri mkuu ajiuzulu na uchaguzi uitishwe kabla ya wakati.

"Tukiiachia hali iendelee kama hivi,hatuwezi kuashiria maisha ya watu wangapi zaidi yataangamia" alisema Nattawuk Saikua,mmojawapo wa viongozi wa "Mashati mekundu" wakati wa mkutano na waandishi habari katika kambi ya wapinzani wa serikali mjini Bangkok.

Lakini maafisa wa serikali wamekosoa juhudi za wanachama hao wa baraza la Senet."Serikali inasema,hatuwezi kujadiliana si mpaka maandamano yanamalizika" amesema kwa upande wake,Satit Wongnongtaey ambae ni waziri katika ofisi ya waziri mkuu Abhisit Vejjajiva.

Sharti hilo limekataliwa pia na wakuu wa mashati mekundu.

"Nnashuku kama pendekezo hilo linaweza kumaliza mgogoro wa kisiasa" amesema Kavee Chukitsamen,ambae ni mkurugenzi wa utafiti katika taasisi ya ulinzi ya Kasikorn.Anahisi njia pekee ya kumaliza maandamano ni kupitia hatua ya kijeshi au wapinzani wenyewe wa mashati mekundu waamue kuondoka.

Milio ya risasi imesikika hapa na pale ingawa si ya nguvu ikilinganishwa na siku za nyuma.Mashahidi wanaofuatilizia mapambano kati ya wapinzani na vikosi vya usalama wanaamini,jeshi ndilo linalotumia nguvu:

"Ukitaka kujua nani anafyetua risasi,basi nenda kule.Huko utaona risasi zinatokea wapi.Wamempiga risasi bibi mmoja aliyetoka dukani na mikoba yake ,akielekea nyumbani.Hata ripota mmoja wa kigeni amepigwa risasi."

Flash Galerie Unruhen in Bangkok
Mwanajeshi apiga doria katika eneo moja la mjini BangkokPicha: AP

Jeshi la Thailand linaendelea kuzingira eneo lililotengwa kusini mwa mji mkuu ambako wanaharakati wa upinzani wamepiga kambi zao.Wapinzani kama elfu tano hivi wamejifungia katika eneo la kilomita tatu za mraba katika mtaa wa kibiashara,kati kati ya Bangkok.

Serikali iliwapa muda wapinzani wayahame maeneo hayo wanayoyakalia tangu April tatu iliyopita,hadi jana jioni.Lakini waandamanaji hao wamepuuza amri hiyo na wanajeshi hawakuingilia kati.

Mamia ya wakinamama na watoto wamekusanyika katika hekalu moja kati kati ya eneo linalokaliwa na mashati mekundu-hiyo pengine ndio sababu kwanini wanajeshi hawakuingilia kati.

Watu 67 wameuwawa na 1700 kujeruhiwa tangu mgogoro huu ulipoanza mwezi uliopita.

Mashirika yanayopigania haki za binaadam Amnesty International na Human Rights Watch yamelilaumu jeshi la Thailand kuwafyetulia risasi za kweli raia wasiokua na silaha.

Mwandishi Hamidou Oummilkheir/afp/reuters

Imepitiwa na:Abdul Rahman