1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hatari yatangazwa Tunisia

25 Novemba 2015

Tangazo hilo limetolewa na Rais wa Tunisia Beji Caid Essebsi pamoja na amri ya kutotoka nje usiku katika mji mkuu Tunis, baada ya kulipuka kwenye basi lililowabeba walinzi wa Rais, na kuwauaa watu 13.

https://p.dw.com/p/1HCAw
Hali ya hatari Tunisia
Picha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Rais Essebsi ambaye amelazimika kufuta ziara ya kuelekea Uswisi hii leo ametangaza hali ya hatari itakayodumu kwa siku thelathini baada ya shambulzi hilo la bomu lililowaua watu 13 na kuwajeruhi watu wengine 20. Msemaji wa Serikali ya Tunisia Moez Sinaoui aliuelezea mlipuko huo kuwa ni shambulizi la kigaidi. Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo.

Marakeni imelaani shambulizi hilo na kusema imejitolea kuwasaidia maafisa wa usalama wa Tunisia na uchunguzi kuhusu kisa hicho. Usalama umeimiarisha katika mji mkuu Tunis na wanajeshi na polisi wanashika doria katika mitaa ya mji huo na kufanya ukaguzi katika magari na wapita njia.

Katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Tunis, maafisa wa usalama wanawaruhusu abiria pekee kuingia katika uwanja huo. Shambulizi hilo la jana ndilo shambulizi la tatu kubwa kutokea Tunisia mwaka huu baada ya shambulizi lililotokea katika hoteli ya kutalii ya Sousse mwezi Juni na katika majengo ya makumbusho ya Bardo mwezi Machi.

Ugaidi waathiri utalii

Mashambulizi yote mawili ya awali wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS walidai kuhusika. Afisa wa usalama wa Rais Hichem Gharbi amesema shambulizi kama la jana linalenga dhima ya taifa na wanakabiliwa na changamoto halisi kufuatia shambulizi katikati ya mji mkuu.

Mashambulizi katika hoteli ya watalii yamefanya idadi ya wageni ipungue
Mashambulizi katika hoteli ya watalii yamefanya idadi ya wageni ipunguePicha: picture-alliance/AP Photo/Tunisia TV1 via AP

Gharbi ameongeza kusema kulingana na uchunguzi wa awali, shambulizi hilo dhidi ya walinzi wa Rais lilifanywa na Mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliyekuwa amebeba begi mgongoni na kujiripua baada ya kuingia katika basi hilo.

Tunisia imesifiwa kwa juhudi ilizopiga kurejea katika njia ya kidemokrasia baada ya wimbi la mapinduzi la 2011 lililomng'oa madarakani kiongozi wa kiimla Zine el Abidine Ben Ali.

Hata hivyo nchi hiyo iliyoko kaskazini mwa Afrika, imekumbwa na changamoto kubwa ya kiusalama kutokana na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi ambayo yameathiri kitega kikubwa cha uchumi wa tafa hilo - utalii. Zaidi ya watunisia 3,000 wamekwenda nchini Iraq, Syria na katika nchi jirani ya Libya kujiunga na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali kama wapiganaji.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman