1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wasi wasi yaongezeka Iraq

24 Agosti 2014

Mashambulio ya mabomu mjini Baghdad na mji wa kaskazini wa Kirkuk yamesababisha vifo vya takriban watu 42 nchini Iraq Jumamosi(24.08.2014) wakati serikali inachunguza shambulio baya kabisa dhidi ya msikiti wa Wasunni.

https://p.dw.com/p/1Czrc
Irak Anschlag in Kirkuk 23. August
Shambulio la bomu katika mji wa kirkukPicha: Marwan Ibrahim/AFP/Getty Images

Hali hiyo imeongeza wasi wasi wa kimadhehebu nchini Iraq huku kukiwa na hatua tete za mpito kisiasa.

Katika mji ambako kuna utajiri mkubwa wa mafuta wa Kirkuk , mji ambao unabishaniwa kwa muda mrefu baina ya serikali mjini Baghdad na serikali ya kimkoa ya Wakurdi , mabomu matatu yaliripuka katika eneo la kibishara , na kuuwa watu 31 na wengine kadhaa wamejeruhiwa, mkuu wa jeshi la polisi mjini Kirkuk Tarhan Abdel-Rahman amesema.

Irak Anschlag in Kirkuk 23. August
maiti zikiondolewa kutoka katika eneo la tukioPicha: Marwan Ibrahim/AFP/Getty Images

Mtu mmoja aliyeshuhudia amesema amesikia "mripuko baina ya magari, na kisha wakaanza kuwatoa watu waliofariki kutoka mahali hapo wakati watu walikuwa wakiungua ndani ya maduka na magari." Mtu huyo aliyeshuhudia hakutaka kutajwa jina lake kwa hofu ya kulipiziwa kisasi.

Wimbi la mashambulizi mjini Baghdad

Mjini Baghdad , mshambuliaji wa kujitoa muhanga hapo mapema aliendesha gari yake iliyojaa miripuko na kuligonga katika lango kuu la makao makuu ya upelelezi katika wilaya ya Karrada, na kuuwa raia sita pamoja na walinzi watano wa usalama, amesema afisa wa polisi. Amesema watu wengine 24 wamejeruhiwa.

Afisa wa hospitali alithibitisha idadi hiyo ya watu waliouwawa. Maafisa wote walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwa kuwa waharuhusiwi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Mashambulio hayo yamekuja baada ya spika wa bunge Salim al-Jabouri kusema kuwa kamati ya maafisa wa usalama na wabunge inachunguza shambulio la Ijumaa dhidi ya msikiti wa kijiji katika jimbo la Diyala, kaskazini mashariki mwa mji mkuu , shambulio lililouwa zaidi ya watu 60.

Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kuwasilishwa katika muda wa siku mbili.

Haijafahamika iwapo shambulio hilo katika kijiji cha Imam Wais limefanywa na wanamgambo wa Kishia ama wapiganaji kutoka kundi la Taifa la Kiislamu, ambao wamekuwa wakisonga mbele katika maeneo hayo yaliyochanganyika Wasunni na Washia katika jimbo la Diyala na wamekuwa wakijulikana kwa kuwauwa Wasunni wenzao ambao wanakataa kukubaliana na tafsiri yao kali ya sharia za Kiislamu.

Irak Anschlag in Kirkuk
Shambulio katika mji wa KirkukPicha: MARWAN IBRAHIM/AFP/Getty Images

Tangu mapema mwaka huu , Iraq imekumbana na mauaji yanayofanywa na kundi lenye itikadi kali la Taifa la Kiislamu pamoja na wanamgambo washirika wao wa Kisunni, ambao wamekamata maeneo makubwa katika upande wa magharibi na kaskazini nchini humo.

Kundi hilo limeukamata mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq wa Mosul mwezi Juni, na limetangaza taifa la Kiislamu, ama Khalifa , katika ardhi chini ya udhibiti wake katika nchi za Iraq na Syria.

Shambulio dhidi ya msikiti

Maafisa wa usalama wa eneo la Diyala wamesema shambulio la Ijumaa lilianza kwa shambulio la kujitoa muhanga karibu na eneo la kuingilia msikitini hapo. Watu wenye silaha baadaye walivamia jengo hilo na kuanza kufyatua risasi kwa waumini. Kiasi ya watu 64 wameuwawa, ikiwa ni pamoja na wanamgambo wanne wa Kishia ambao walikanyaga mabomu yaliyowekwa na wanamgambo wakati wakiharakisha kufika katika tukio wakiwa na majeshi ya usalama.

Waziri mkuu mteule Haidar al-Abadi , ambaye ni mshia, ameshutumu shambulio hilo na kutoa wito kwa "raia kuungana na kutotoa nafasi kwa maadui wa iraq ambao wanajaribu kuchochea mivutano".

Frank-Walter Steinmeier SPD Bagdad Irak Ministerpräsident Haidar al-Abadi
Waziri mkuu mteule Haidar al-Abadi wa Iraq(kulia) na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa

Kundi la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeliita shambulio la Ijumaa kuwa ni "mauaji ya kiholela", na kusema maafisa wa Iraq "wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina".

Maafisa wa jeshi na polisi wamesema shambulio hilo dhidi ya msikiti wa Musab bin Omair katika jimbo la Diyala limekuja baada ya wanamgambo wa Kishia kuuwawa katika mapigano, wakati duru nyingine zinasema limekuja baada ya shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara karibu na moja kati ya vikosi vya doria.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri:Gakuba Daniel