1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hariri aiona Syria haina makosa juu ya kifo cha Babaake

7 Septemba 2010

Waziri mkuu wa Lebanon, Saad al-Hariri,amekiri kwamba muungano anaouongoza na unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, ulifanya haraka kuituhumu Syria kwa kuuliwa baba yake, waziri mkuu wa zamani, Rafik al-Hariri.

https://p.dw.com/p/P64G
Waziri mkuu Saad Al Hariri alipokutana kwa mara ya kwanza na Rais Assad wa Syria tangu kuuwawa kwa hayati babaake.Picha: AP

Hayo yalikuwa katika matamshi aliyoyatoa kwa gazeti linalosomwa katika nchi nyingi za Kiarabu, asharq al-Awsat, hapo jana. Saad al-Hariri alidai kwamba mashahidi wa uongo waliupa uchunguzi maelekezo ya kugushi.

Matamshi hayo ya Saad al-Hariri yalikuwa ya mwanzo kwa waandishi wa habari baada ya yeye kukutana kwa mara ya tatu na Rais wa Syria, Bashar al-Assad, wiki iliopita. Saad al-Hariri aliyaelezea maingiliano baina ya nchi yake ya Lebanon na Syria kuwa ya kihistoria, akisema kwamba ukurasa mpya umefunguliwa kutokana na kuundwa baraza jipya la mawaziri huko Lebanon mwaka jana. Lakini pia aliashiria kwamba uangalifu lazima uchukuliwe ili kwamba makosa ya zamani yasikaririwe. "Tumetathmini makosa yaliofanywa na ambayo yaliwaumiza watu wa Syria na maingiliano baina ya nchi zao mbili", Saad al-Hariri aliliambia gazeti la asharq al-Awsat. Alisema katika hatua fulani, wao walifanya makosa na kuituhumu Syria kwa kumuua waziri mkuu Rafik al-Hariri. Alisema tuhuma hiyo ilikuwa ya kisiasa na sasa imekwisha.

Der syrische Präsident Baschar el Assad
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: AP

Rafik al-Hariri aliuliwa katika shambulio kubwa la bomu hapo mwaka 2005, na mauaji hayo yamebakia kuwa ni suala tete sana katika Lebanon, licha ya kwamba yalisababisha kutolewa malalamiko ndani kwenyewe Lebanon na kutoka nchi za nje. Wafuasi wa waziri mkuu huyo wakati huo waliituhumu Syria kuwa ilikuwa nyuma ya mauaji hayo, dai ambalo Syria imelikataa kwa nguvu. Pia katika mkasa huo walikufa watu wengine 22. Na baadae Rais Bashar al-Assad alilazimika kuyaondosha majeshi ya nchi yake kutoka Lebanon, hivyo kumaliza karibu miongo mitatu ya majeshi hayo kukaa katika ardhi ya jirani yake mdogo.

Maingiliano baina ya Lebanon na Syria yalipwaya baada ya mauaji hayo, lakini ziara muhimu iliofanywa na Saad al-Hariri huko Damascus mwaka jana iliboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Baraza la mawaziri la Lebanon mwezi uliopita lilimpa jukumu waziri wa sheria, Ibrahim Najjar, kuwashughulikia mashahidi waliotoa ushahidi wa uzushi kwa wachunguzi wa Umoja wa mataifa hapo mwaka 2005. Bwana Najjar amekataa kuzungumzia juu ya uchunguzi wake hadi pale atakapomaliza kuyapitia mafaili ya mashahidi hao.

Kumekuweko na tetesi zinazozidi kwamba mkuu wa mashtaka wa Umoja wa Mataifa, Daniel Bellemare, karibuni atawashtaki wanachama wa kikundi cha Kishia cha Hizbullah kwa mauaji hayo. Jumuiya hiyo ya Hizbullah imekanusha kuhusika na mauaji hayo, na kiongozi wake, Sayyed Nasrallah, ameitaja mahakama ya Umoja wa Mataifa kuwa ni mradi wa Israel; lakini waziri mkuu Saad al-Hariri ameutetea uhuru wa mahakama hiyo. Mabishano juu ya kuaminika kwa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa na uwezekano wa Chama cha Hizbullah kutajwa kwamba kinahusika katika mauaji hayo, kumeitikisa serekali inayolegalega ya Umoja wa Taifa huko Lebanon ambayo inaongozwa na Saad al-Hariri, na ndani yake kuna mawaziri wa kutoka Chama cha Hizbullah. Saad al-Hariri alinukuliwa na gazeti hilo la asharq al-Awsat akisema kwamba mahakama hiyo haifungamani na tuhuma za kisiasa ambazo zilitolewa kwa haraka... mahakama hiyo itaangalia tu ushahidi. Hadi sasa hamna watu walioshukiwa ambao wako ndani.

Katika ziara ya mwishoni ya Saad al-Hariri huko Damascus mwezi wa Julai, alitia saini mikataba kumi na saba ya ushirikiano baina ya Lebanon na Syria.

Mwandishi: Othman Miraji

Mhariri: Josephat Charo