1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatun, muhanga mwengine wa 'mauaji ya heshima' Ujerumani

Daniel Gakuba
31 Mei 2017

Kosa alilolifanya Hatun Sürücü lilikuwa kuhalifu utamaduni na maadili kwa mtazamo wa familia yake, akiwa binti wa kwanza katika familia ya Kikurdi iliyohamia Ujerumani miaka ya '70 ikitokea mashariki mwa Uturuki.

https://p.dw.com/p/2dsyE
Deutschland Gedenkstein für  Hatun Sürücü
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Baada ya kubaleghe, Hatun alizidisha uasi kwa familia yake. Baba yake alimuachisha shule, na alipotimiza umri wa miaka 16 aliozwa kwa nguvu kwa binamu yake nchini Uturuki. Alipata mimba, lakini baadaye wakaachana kutokana na ugomvi. Hatun alirudi mjini Berlin na baada ya kujifungua mtoto wa kiume alihamia katika makazi ya mabinti waliojifungua wakiwa na umri mdogo. Alihitimu chuo na kupata cheti, na kuajiriwa kama mwalimu wa mafundi umeme.

Ingawa kwa nje, maisha yake yalionekana kutokuwa na kikwazo, lakini machoni mwa wazazi na kaka zake, alikuwa amekiuka kila mwiko. Hali ya kwamba Hatun aliendeleza maisha yake kwa uhuru, wakati huo huo akiendelea kuwasiliana na familia yake ilimchimbia kaburi. Jioni ya tarehe 7 Februari 2005, kaka yake Ayhan alimfuata nyumbani kwake. Walikuwa na ugomvi. Walipokuwa wakienda kwenye kituo cha basi, Ayhan alimpiga Hatun risasi tatu kichwani.

Ukosevu wa maelewano na kuvumiliana

Tukio hilo liliibua mjadala uliojawa na hisia kuhusu 'mauaji ya kulinda heshima', hususan kwa sababu tayari mauaji kama hayo yalikuwa yakiongezeka mjini Berlin wiki chache kabla.

Mauaji ya Hatun Sürücü yaliangaziwa zaidi baada ya wanafunzi watatu wa darasa la nane katika shule ya mjini Berlin kuyaunga mkono katika mjadala.

10. Todestag von Hatun Sürücü
Mashada ya mauwa yakiwa yamewekwa kwenye eneo alilouawa Hatun mwaka 2005.Picha: picture-alliance/dpa/L.Schulze

Mwalimu mkuu wa shule hiyo aliandika katika barua yake ya wazi kwamba kulikuwa na kauli kama ''aliyatafuta mwenyewe, malaya aliishi kama Mjerumani''. ''Wanafunzi hawa wanahujumu amani katika maisha ya shule, hatuvumilii uhamasishaji unaopinga uhuru'', aliandika mwalimu huyo.

Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ujerumani wakati huo, Horst Köhler, alijibu akisema ''kuelewa vibaya maana ya kuvumiliana, kuishi pamoja au ukosefu wa ujasiri, havipaswi kuzidi nguvu misingi ya kuishi pamoja katika jamii yetu."

Ekin Deligöz, aliyekuwa mbunge wa Chama cha Kijani katika Bunge la Shirikisho, na Sidar Demirdogen, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha wanawake wahamiaji, walionya dhidi ya kuwachukulia wahamiaji wote kwa mtazamo mmoja.

Deligöz alitoa hoja kuwa badala ya kuimarisha adhabu, watoto wapelekwe shule mapema na kwa mrefu, kujifunza lugha na mienendo sahihi ya kijamii. Alitaka pia mafundisho ya Kiislamu yasiachiwe kuendeshwa bila ukaguzi katika jamii za Waislamu.

Kuhusika kwa kaka wa muuwaji

Mahakamani, Ayhan Sürücü alisema kuwa alichukizwa na maisha ya dada yake ya mtindo wa kimagharibi na kwamba alitaka kuhifadhi heshima ya familia. Alihukumiwa kifungo cha miaka 9 na miezi mitatu mnamo Aprili mwaka 2006.

Hata hivyo, watuhumiwa wenzake wawili, ambao inaaminika walimhamasisha Ayhan kumuuwa dada yao, waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi dhidi yao.

Mwezi Agosti 2007, Mahakama ya Shirikisho ilibatilisha uamuzi wa kesi hiyo, lakini kesi haikuendeshwa upya nchini Ujerumani, kwa sababu tayari walikwishahamia Uturuki.

Kusitasita kwa mahakama ya Uturuki

Ilichukuwa miaka minane kwa Uturuki kuwafikisha mahakamani kaka hao, Alpaslan na Mutlu Sürücü. Ujerumani ilifanya tafsiri ya mafaili kadhaa kwa lugha ya Kituruki na kuyakabidhi kwa vyombo vya sheria vya Uturuki. Hata kuanza kwa kesi hiyo kulitokana na juhudi za mwanasheria wa mjini Berlin, Abdurrahim Vurul, ambaye katika mahojiano na Deutsche Welle, alilalamika akisema Uturuki haitoi ushirikiano wa kutosha.

"Kesi ya kaka hao imeendeshwa kimataifa kwa miaka mingi, kitu kisichoeleweka ni kwamba hawajahukumiwa nchini Uturuki. Mwanzoni mwa 2009, niliandika barua ya malalamiko kwa mwendesha mashitaka wa Uturuki, nikiainisha hali ya kisheria na ya ushahidi nchini Ujerumani, na kutaka kesi iendeshwe huko Uturuki, lakini ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Uturuki haikutaka kuchukua hatua yoyote wakati huo."

Baada ya kutumikia kifungo chake nchini Ujerumani, Ayhan alirudishwa nchini Uturuki, ambako akitoa ushahidi katika kesi ya kaka zake, alisema alimuua dada yao peke yake. Na kuhusu sababu ya kumuuwa dada yake, mara hii alibadilisha kauli. Hakusema kuwa alichukizwa na mtindo wa maisha ya dada yake, bali alisema alirukwa na akili.

Kulingana na maafisa wa Berlin, Ayhan kamwe hakuonyesha kujutia mauaji aliyoyafanya, badala yake aliyaonea fahari. Katika kitabu kiitwacho ''Heshima Iliyopotea- Njia Potofu ya Familia ya Sürücü'' kilichoandikwa na Matthias Deiss na Joachim Goll, Ayhan anajaribu kuhalalisha ''mauaji ya heshima'' akidai yapo katika kila utamaduni.

'Mauaji ya heshima' bado ni tatizo kubwa

Mwanaharakati wa haki za wanawake, Rukiye Leyla Süren, anasema ni jambo jema kwamba mwendesha mashitaka katika kesi iliyoendeshwa Uturuki, alikiri kuwa 'mila' ni suala kubwa katika masuala ya uhalifu.  

Anasema kuwepo hali hiyo mpya ni matokeo ya mapambano ya muda mrefu kwa ajili ya haki za wanawake nchini Uturuki. Bado anachukulia mauaji dhidi ya wanawake kuwa tatizo kubwa katika nchi hiyo, baada ya hali hiyo kama ilivyokuwa kabla.

Deutschland Urteil im Prozess um «Ehrenmord» an Schwester
Alpalan Sürücü (kulia), mmoja wa kaka wa Hatin, walioshitakiwa kwa mauaji ya dada yao. Picha: picture-alliance/dpa/S. Kugler

Kulingana na takwimu za utafiti wa mwaka 2014, wastani wa wanawake 6 huuawa na familia zao au waume zao kila wiki nchini Uturuki. 

Mwezi Januari, mwanasheria Abdurrahim Vurul alielezea matumaini kuwa ushirikiano wa kisheria unaweza kuimarika siku za usoni kati ya Uturuki na Ujerumani. Anasema sio sahihi kujenga mtazamo kwamba "mtu anaweza kukwepa adhabu kwa kuikimbia nchi."

Lakini hayo yalikuwa kabla ya mzozo wa hivi karibuni baina ya nchi hizo, uliotokana na tofauti zilizoibuka wakati wa kampeni za kura ya maoni ya kuifanyia mageuzi katiba ya Uturuki, na mgogoro kuhusu kambi ya wanajeshi wa Ujerumani iliyoko Incirlik, Uturuki.

Mwandishi: Hasselbach, Christoph
Tafsiri: Gakuba, Daniel
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman