1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton awasili mjini Bangkok, Thailand akielekea Phuket.

Kabogo Grace Patricia21 Julai 2009

Akiwa nchini Thailand, kabla ya mkutano wa usalama wa ASEAN, Clinton amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abhisit Vejjajiva.

https://p.dw.com/p/Iugo
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: picture alliance / landov


Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, amesema kuwa nchi yake ina wasi wasi kuhusu ushirikiano wa kijeshi uliopo kati ya Korea Kaskazini na Myanmar. Bibi Clinton ameyasema hayo leo alipowasili mjini Bangkok, akielekea Phuket, Thailand, kuhudhuria mkutano juu ya usalama wa nchi za Jumuiya ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN.

Akizungumza baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Thailand, Abhisit Vejjajiva, Bibi Clinton amegusia utawala wa kijeshi wa Myanmar, zikiwemo tuhuma kwamba jeshi la nchi hiyo linawanyanyasa wasichana wadogo. Wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili ulianza baada ya meli ya kijeshi ya Marekani ilipoanza kufatilia nyendo za meli ya Korea Kaskazini iliyokuwa ikidaiwa kuelekea nchini Myanmar mwezi uliopita.

Mkutano huo wa Alhamisi unaangaliwa kama kuna mwelekeo wowote wa sera za Marekani kwa Korea Kaskazini na Myanmar kubadilika. Bibi Clinton amesema wanachoangalia wao ni kuwa na uhusiano imara ulio bora baina yake na Myanmar, endapo nchi hiyo itafanya marekebisho kadhaa, yakiwemo ya kisiasa, kuacha ghasia dhidi ya wananchi wake wenyewe, hasa wasio na sauti na kuangaliwa vizuri wafungwa wa kisiasa, akiwemo kiongozi wa upinzani, Aung San Suu Kyi.

Bibi Clinton amesema kuwa ushirikiano kama huo unaweza kudidimiza uhusiano wa nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia. Myanmar na Korea Kaskazini zinazokosolewa na jumuia ya kimataifa kwa kukiuka haki za binaadamu, zilirejesha uhusiano wake mwaka 2007 baada ya mpasuko uliodumu kwa miaka 24.

Aidha, maafisa wa Marekani wamesema kuwa Bibi Clinton atakutana kwa nyakati tofauti na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Korea Kusini, China, Japan na Russia. Hata hivyo, Bibi Clinton hatokutana kwa wakati tofauti na ujumbe wa Korea Kaskazini. Nchi hiyo, inayoonekana kuwa tishio kutokana na mpango wake wa nyuklia, imekataa kurejea katika meza ya mazungumzo ya pande sita ambayo kwa kiasi kikubwa yanalenga kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la DPA, Korea Kaskazini ndiyo nchi pekee iliyokataa kumpeleka Waziri wake wa Mambo ya Kigeni kuhudhuria mkutano huo wa kiusalama, na badala yake nchi hiyo itawakilishwa na maafisa watano wa ngazi ya chini katika mkutano huo utakaoshirikisha mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka makundi 27 wanachama. Akiwa nchini Thailand, Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani atasaini mkataba wa ushirikiano na uhusiano mwema na nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia. Utawala uliopita wa George Bush, ulikataa kusaini mkataba huo unaojulikana kama TAC.

Wakati hayo yakijiri, kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Yang Jiechi, amesema hana mipango ya kukutana na waziri mwenzake wa Australia, Stephen Smith, kando na mkutano huo wa Thailand wa masuala ya kiusalama. Mapema leo, Waziri Smith alisema kama atakutana na Waziri Yang, anataka kuzungumzia hatua ya kushikiliwa wafanyakazi wa kampuni ya madini ya Rio Tinto.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP/DPAE)

Mhariri: Othman Miraji