1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton Mashariki ya Kati

3 Novemba 2009

Je, Bi Clinton atafaulu kuwapoza moyo waarabu ?

https://p.dw.com/p/KMHF
Hillary Rodham Clinton na Benjamin Netanyahu .Picha: AP

Waziri wa nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, atazuru Misri hapo kesho ili kuonana na rais Hosni Mubarak katika juhudi zake za kuanzisha upya mazungumzo ya amani kati ya Israel na wapalestina.

Bibi Clinton alikuwa Marrakesh,Morocco hapo jana ikiwa sehemu ya mkutano wake na mawaziri wa nje wa nchi za kiarabu. Katika mazungumzo hayo na viongozi wa nchi za kiarabu, Bibi Clinton, amejaribu kuwatuliza moyo baada ya kuwakasirisha kwa pongezi alizompa mwishoni mwa wiki waziri mkuu Benjamin Netanyahu kwa kujitolea tu kupunguza ujenzi wa maskani za wayahudi-suala linalozusha utata katika kuanzisha upya mazungumzo.

Utawala wa rais Barack Obama unapaswa sasa kutunga mkakati mpya ili kuanzisha tena mazungumzo ya amani kati ya Israel na Waarabu. Hii ni baada ya kupoteza imani kwa kurejesha ulimi wake katika dai lake kuwa Israel ikomeshe ujenzi wa maskani za walowezi wa kiyahudi katika ardhi za Wapalestina-wachambuzi wanasema.

Rais Barack Obama amewavunja moyo Wapalestina na Waarabu wengi waliomtarajia kutekeleza tangu ahadi zake za awali za kuichukulia Israel msimamo mkali juu ya ujenzi wa maskani na za mipaka ili kutengeneza usuhuba na ulimwengu wa kiislamu-wachambuzi hao waliongeza.

Wakati wa ziara yake hii ya sasa ya Mashariki ya kati ambayo kesho itamchukua Cairo,Misri, kwa mkutano na rais Hosni Mubarak, waziri wa nje Bibi hillary Clinton,

akijaribu kuwapoza moyo waarabu waliokasirikiana naye mwishoni mwa wiki aliposifu kujitolea kwa waziri mkuu Netanyahu wa Israel kupunguza ujenzi wamaskani kuwa ni hatua "isio na kifani". Bibi Clinton alidai kuwa, serikali ya marekani hatahivyo, inaendelea kupinga ujenzi wa maskani tena kwa nguvu kama hapo kabla.

Akilikanusha dai hilo la Bibi Clinton, Bw.Aaron David Miller, aliekuwa mshauri wa juhudi za amani za Mashariki ya Kati katika serikali zilizopita za Marekani, alisema ,

"Netanyahu ametamba kwa werevu wake. Ametuzunguka kwa mbinu zake ......Amemtia munda Kiongozi wa Palestina, Mahmud Abbas, na ameweza kulikatalia dola kuu tena bila kupatwa na athari zozote."

Miller akaongeza kusema kuwa`, kiroja cha mambo ni kuona utawala ulioanza kwa siasa kali mbele ya Israel na kuwahurumia kidogo waplestina, sasa imewageukia wapalestina.Rais wa Palestina, Mahmud Abbas alimwambia jana mjumbe wa Marekani katika Mashariki ya kati ,George Mitchell mjini Amman,Jordan kwamba, Wapalestina hawatarejea kwenye mazungumzo ya amani na Israel hadi kwanza Israel, imekomesha ujenzi wa maskani za walowezi katika ukingo wa magharibi.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za kiarabu-Arab League-Amr Mussa, aliituhumu jana Israel kuchafua juhudi za Marekani kuanzisha upya mazungumzo ya Mashariki ya kati na akaungamkono msimamo wa wapalestina wa kutorejea mezani kuanza tena mazungmzo na Israel hadi imekomesha ujenzi wa maskani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE/DPAE

Mhariri: Abdulrahman