1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya nguruwe yasambaa ulimwenguni

29 Aprili 2009

Homa ya nguruwe iliyozuka nchini Mexico inaendelea kusambaa kote ulimwenguni.Watu kadhaa wameripotiwa kuambukizwa virusi vya homa hiyo hatari huko Israel na New Zealand nako Marekani watu 64 wameripotiwa wameambukizwa

https://p.dw.com/p/HgB9
Wakazi wote wa Mexico walazimika kuvaa vichuja pua.Picha: AP

Uchunguzi unaendelea barani Ulaya ,Asia na Latin Amerika.Mpaka sasa jumla ya watu 150 wameripotiwa kufariki baada ya kuambukizwa homa hiyo hatari nchini Mexico pekee na watu wengine 1600 wameambukizwa virusi hivyo.

Watu wanne wameambukizwa virusi vya homa hiyo Uhispania na Uingereza.Idara za afya katika mataifa mengine barani Ulaya ziko katika harakati za kuwapima watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa homa hiyo.Hapa Ujerumani watu saba waliolazwa kwenye hospitali kadhaa katika majimbo ya Bavaria,North-Rhine Westphalia na mji wa Hamburg wanaendelea kufanyiwa uchunguzi.

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetahadharisha kuwa hali hiyo imefikia awamu ya nne ambapo maambukizi kati ya wanadamu yanaweza kutokea.Hata hivyo shirika hilo limesisitiza umuhimu wa kuwa chonjo pasipo kufunga mipaka ya nchi husika.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya /RTRE,AFPE