1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya rais Bashar al Assad haijawaridhisha wananchi wake

20 Juni 2011

Waandamanaji wameteremka majiani kote nchini Syria hii leo kukosoa hotuba iliyotolewa na rais Bashar al-Assad wanayosema haijibu madai ya umma ya kuleta mageuzi ya kina ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/11fge
Rais Bashjar al Assad wa SyriaPicha: dapd/Syrian TV

Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa katika chuo kikuu cha mjini Damascus na kutangazwa moja kwa moja na televisheni,rais Bashar al Assad ameahidi chaguzi za bunge zitaitishwa mwezi Agosti na mpango wa mageuzi utaandaliwa hadi ifikapo September mwaka huu.

Rais Assad amewalaumu wale anaowataja kuwa "waharibifu" miongoni mwa waandamanaji wanaodai ukome utawala wake wa miaka 11,akihoji wametumwa na nchi za nje wachochee fujo nchini.

"Waharibifu,ambao ndio chanzo cha machafuko,ni kundi dogo linalojaribu kuwashawishi wananchi walio wengi wa Syria,ili waweze kulifikia lengo lao."Amesema rais Assad katika hotuba yake hiyo iliyodumu zaidi ya saa moja.

Katika wakati ambapo vikosi vya Syria vimewekwa katika maeneo yanayopakana na Uturuki,kaskazini magharibi ya nchi hiyo,na kuzuwia mikururo ya watu wanaoyapa kisogo madhila,rais Bashar Al Assad amewatolea mwito watu elfu kumi waliokimbilia Uturuki warejee nyumbani.

Syrien Flüchtlinge Türkei Saleh Aufstand Grenze Soldat
Mwanajeshi wa Uturuki anaangalia wasyria wakivuka mpaka na kuingia UturukiPicha: AP

Hotuba hiyo ya tatu ya aina yake tangu maandamano dhidi ya serikali yake yalipoanza kati kati ya mwezi March mwaka huu,haijawaridhisha waandamanaji.Walianza kuteremka majiani katika vitongoji vya mjini Damascus ,na katika miji kadhaa ya Syria wakimwita "muongo" huku wengine wakisema hawatozungumza na makatili.

"Watu walikuwa wakitaraji angesema jambo la maana ambalo lingepelekea vifaru na vikosi kuondoshwa majiani.Wamevunjika moyo ndio maana wameteremka tena majiani kuandamana,mara tu baada ya Assad kumaliza hotuba yake." amesema mwanaharakati mmoja wa amji wa mwambao wa Latakia .

Rais Bashar Al Assad amesema anahuzunishwa na idadi ya wahanga wa pande zote mbili,raia na vikosi vya usalama na kuwataja kuwa "mashahidi.

Hakuzungumzia lolote kuhusu matumizi ya nguvu yaliyokithiri yanayofanywa na wanajeshi,idara ya upelelezi na kadhalika.Na wala hajasema kama visa kama hivyo vitakoma seuze kuzungumzia uwezekano wa kujiuzulu au kubadilishwa serikali.

Mtaalam wa masuala ya kisiasa kutoka Qatar Faisal Braisad anasema

"Watu wanataka serikali iwarejeshee hadhi yao,uhuru na nafasi za kujiendeleza."

EU Außenminister Treffen 10.05.2010 Catherine Ashton
Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa Ulaya bibi Catherine AshtonPicha: Picture alliance/dpa

Wakati huo huo Umoja wa ulaya umetangaza kuzidisha makali ya vikwazo dhidi ya utawala wa Syria na kuonya itibari ya rais Bashar al Assad kuendelea kusalia madarakani itategemea ahadi alizotoa za kufanya mageuzi.

Katika mkutano wao mjini Luxembourg,mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa umoja wa Ulaya wa melitolea mwito pia baraza la usalama la Umoja wa mataifa liwasaidie katika juhudi zao hizo na kukosoa onyo la Urusi la kutaka kutumia kura ya turufu kupinga azimio lolote dhidi ya Syria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir,afp,reuters

Mhariri:Yusuf Saumu