1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW lataka uchunguzi ufanyike Sudan

Saumu Mwasimba
11 Februari 2019

Baada ya kuenea madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya serikali shirika la Human Rights Watch lautaka Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuchunguza madai hayo.

https://p.dw.com/p/3DAD4
Sudan Proteste gegen Präsident Al-Baschir
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutolea mwito Umoja wa Mataifa kuchunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama vya Sudan dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Sudan imekumbwa na maandamano ya nchi nzima ya watu wanaoipinga serikali tangu mwezi Desemba 19 mwaka uliopita. Maandamano hayo yalichochewa na hatua ya kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu pamoja na ukosefu wa chakula lakini baadaye yakageuka haraka sana na kuwa harakati za kumtaka rais Omar al-Bashir aondoke madarakani.

Sudan Khartoum - Sudans Präsident - Omar Bashir
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/M. Khidir

Taarifa ya Human Rights Watch iliyotolewa Jumatatu 11.02.2019 imetowa mwito kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuzungumzia katika mkutano wake wa mwezi machi kuhusu mgogoro wa Sudan. Shirika hilo lenye makao yake mjini New York nchini Marekani limesema kwamba limepata mkanda wa video  unaoonesha vikosi vya serikali vikitumia nguvu za kupindukia dhidi ya wanancxhi na mateso mengine ya kushtusha dhidi ya waandamanaji.

Wanaharakati wanasema kiasi watu 57 wameuwawa katika maandamano hayo wakati serikali katika takwimu yake iliyoitowa hivi karibuni ikisema watu 30 ndio waliouwawa ingawa pia kinachofahamika ni kwamba idadi hiyo ya waliouwawa haijawahi kubadilishwa kwa siku kadhaa. Siku ya Jumapili inatajwa kwamba vikosi vya usalama vya serikali ya Sudan vilifyetua gesi za kutowa machozi dhidi ya waandamanaji kuwatawana mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika wengi wakiwa ni wasichana waliokuwa wakipinga hatua ya kuzuiliwa kwa wanawake waliokamatwa wakati wa maandamano yaliyopita.

Sudan Proteste gegen Präsident Al-Baschir
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Waandamanaji wamesikika wakipiga kelele za kusifu harakati za mapambano ya wanawake wakisudan wanaopigania kumuondowa madarakani rais Omar al Bashir. Inatajwa kwamba vikosi vya serikali katika mji wa Omduman ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini humo unaopakana na mji mkuu Khartoum walionekana wakiwakamata wanawake na kuwapakia kwenye magari manne ya wazi Waandamanaji hao walikuwa wakijaribu kuandamana kuelekea gereza kubwa la wanawake  kabla ya vikosi hivyo kuwavamia. Pamoja na hayo rais Bashir na maafisa wake wa ngazi ya juu wamekuwa wakitumia lugha ya kutaka zaidi maridhiano  kuhusu maandamano hao ikiwemo  ahadi ya kuwatoa jela waandamanaji waliofungwa ingawa pia vikosi vya usalama vimekuwa vikiendelea kuivunja mikutano na maandamano  na kuwakamata watu.

Mwandishi:Saumu Yusuf

Mhariri: Josephat Charo