1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Wanamgambo wafanya uhalifu wa kibinaadamu, Kongo

Saumu Mwasimba
13 Juni 2023

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wanamgambo wanaungwa mkono na Rwanda wa M23 wamefanya uhalifu wa kibinadamu katika eneo tete la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4SWsM
Human Rights Watch | Logo
Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Taarifa ya shirika hilo la Human Rights Watch iliyotolewa leo Jumanne imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwaorodhesha viongozi wa kundi hilo la wanamgambo, pamoja na maafisa wa Rwanda katika orodha yake ya watu waliowekewa vikwazo.

Mtafiti kuhusu Afrika wa shirika hilo lenye makao yake jijini New York Marekani, Clementine de Montjoye amesema mauaji ya  kikatili na ubakaji umepewa nguvu na uungaji mkono wa kijeshi wa makamanda wa Rwanda, kwa kundi hilo la wanamgambo wa M23.

Shirika hilo pia limesema limeorodhesha visa vinane vya mauaji ya kinyume cha sheria ya watu wanane pamoja na visa 14 vya ubakaji uliofanywa na wapiganaji wa M23. Rwanda imekanusha madai ya Human Rights Watch ikisema haitotishwa na kampeini ya kueneza taarifa zisizo za kweli na kuiondowa kwenye dira ya kuangazia juhudi za kutafuta amani zinazoendelea.