1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda msanii Bill Cosby akaelekea gerezani.

27 Aprili 2018

 Baada ya miongo kadhaa ya minong´ono, uchunguzi na kesi kufuatiliwa kwa karibu, huenda msanii wa Kimarekani  Bill Cosby akaelekea gerezani akiwa na umri wa miaka 80 kwa makosa ya udhalilishaji wa kingono.

https://p.dw.com/p/2wn3Q
USA Prozess Bill Cosby, sexueller Missbrauch
Picha: Reuters/B. McDermid

Msanii huyo wa vichekesho alipatikana na hatia  siku ya Alhamisi yya kumpa dawa za kulevya na kumdhalilisha kingono mfanyikazi wa Chuo Kikuu cha Temple Andrea Constand katika makazi yake yaliyoko Philadelphia mwezi Januari, 2004. 

Wanasheria wanawake  wameutaja uamuzi huo kuwa wa kihistoria. Vuguvugu kwenye mitandao lenye jina #MeToo, limethibitisha kuwa waliokuwa wakimtuhumu Cosby siku zote hawakuwa na makosa: Haiba yake ya uungwana sasa  imevurugwa .

Lili Bernard, aliyesema kuwa Cosby alimdhalilisha kingono kabla ya kumpa nafasi katika kipindi chake maarufu cha "The Cosby Show" mwaka 1992, alijawa na jazba katika mahakama kiasi cha kugonga kichwa chake bila ya kukusudia kwenye meza iliyokuwa mbele yake.

Bill Cosby akiondoka mahakamani
Bill Cosby akiondoka mahakamaniPicha: picture-alliance/AP Photo/The Philadelphia Inquirer/D. Maialetti

"Nimezidiwa na furaha, alisema Bernard nje ya mahakama huku akidondokwa na machozi." Je, nimeamka? Huu ni muujiza."

Zaidi ya wanawake 60 wamelalama kuhusu Cosby

Uamuzi huo, wa kwanza unaomhusisha msanii anayetambulika katika kipindi cha  #MeToo, inahujumu sifa za  msanii mkubwa aliyevuka mipaka ya rangi katika  jukwaa la kuigiza la  Hollywood na kubobea kwenye Televisheni .

Ni moja ya kesi iliotokana na  visa vilivyowakumbuka zaidi ya wanawake 60 waliodai kuwa Cosby aliwapa dawa za kuelevya na kisha kuwadhalilisha kingono kwa kipindi cha miongo mitano, lakini ambao kadhia zao hazikuaminika ama zilipuuzwa kabla ya kuanza kampeni kwenye mitandao ya kijamii yenye anwani #MeToo iliyoangazia dhulma za kingono zilizotekelezwa na wanaume wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

Cosby alitumbua macho maelezo ya jaji yakisomwa, lakini baadaye akapaza sauti akimpinga jaji Kevin Steele baada ya mwendesha mashtaka kutaka Cosby apelekwe gerezani mara moja.

Mwendesha mashtaka aliambia mahakama kuwa Cosby ana ndege ya kibinafsi na huenda akiachiliwa akatoroka. Cosby alikanusha kwa hasira kuwa anamiliki ndege na kumtusi mwendesha mashtaka .

Cosby alishtakiwa kwa makosa matatu ya udhalilishaji wa kingono, kila moja likiwa na kifungo cha kati ya miaka mitano hadi 10 gerezani.

Mashtaka hayo huenda yakajumlishwa ama kuunganishwa kwa ajili ya hukumu, lakini ikizingatiwa umri wa Cosby, kifungo chochote kinamaana kuwa huenda akafia gerezani.

Cosby amesema kuwa atakata rufaa

USA Bill Cosby Prozess in Norristown
Bill Cosby anakabiliwa na makosa matatu ya udhalilishaji wa kingonoPicha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

Utekelezaji wa kifungo chake huenda ukafanyika katika kipindi cha miezi mitatu. Kabla ya hayo Cosby lazima afanyiwe uchunguzi kuthibitisha iwapo kuwa ni mtumiaji wa nguvu wa dhulma za kingono. Aidha atajiandikisha kuwa mkosaji wa kingono kwa kuzingatia sheria za Megan.

Jopo la wanaume saba na wanawake watano lilishauriana kwa muda wa masaa 14 kabla ya kutoa uamuzi dhidi ya Cosby.

Constand- 45, mfanyikazi wa Chuo Kikuu cha Temple, alisema Cosby alimlemaza kwa kumpa tembe tatu kisha akakosa fahamu, kisha akamdhalilisha kingono kwa kutumia vidole vyake alipokuwa amelala hana nguvu za kukubali ama kukataa. Cosby anadai kuwa kitendo hicho kiliafikiwa na wote.

Cosby aliupungia mkono umati ambao ulikuwa nje ya mahakama na kuingia kwenye gari lake na kuondoka bila ya kusema chochote. Wakili wake Tom Mesereau alitangaza, "vita havijakamilika" na kusema kuwa atakata rufaa.

Mawakili wa upande Cosby wakiongozwa na Mesereau, aliyeshinda kesi dhidi ya Michael Jackson kuhusu kuwadhalilisha watoto kingono, walishambulia Constand wakati wa kesi hiyo huku wakimuita muongo ambaye alimsingizia Cosby kwa lengo la kutaka kuwa tajiri.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap, Ape

Mhariri: Mohammed Abdu-Rahman