1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya muandishi habari

23 Oktoba 2008

Muandishi habari wa Afghanistan ahukumiwa adhabu ya miaka 20 gerezani.

https://p.dw.com/p/FfRz

Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu ,yamemtaka Rais Hamid Karzai na watawala nchini Afghanistan, kumuacha huru muandishi-habari wa kiafghanistan PERWIZ KAMBAKHSH-aliehukumiwa kifungo cha miaka 20 korokoroni kwa kukutikana na hatia ya "kukufuru".

Mkurugenzi wa eneo la Asia-Pacifik wa Shirika la haki za binadamu la AMNESTY INTERNATIONAL , anadai hakuna sababu zozote za kisheria kwanza kumkuta na hatia na pili kumpitishia adhabu kama hiyo.

"Wakati ni uzuri kuona mshtakiwa hakabiliwi tena na adhabu ya kifo,anapasa aachwe huru haraka."-alidai Sam Zarifi wa Amnesty International.

Mshtakiwa Kambakhsh ni mwanafunzi wa uwandishi habari katika chuo kikuu cha Balkh na ni ripota wa gazeti la JAHAN-E-NAW-maana yake Ulimwengu mpya.

Kijana huyu alikamatwa kotoba 27,2007 na akashtakiwa kwa makosa ya "kukufuru" na kueneza taarifa zenye kuumbua uislamu."

Watawala wa Afghanistan upande wao wanadai Kambakhsh alitoa taarifa zilizokuwamo kwenye mtandao wa Internet zilizoelezea mchango wa mwanamke katika jamii za kiislamu na akizieneza taarifa hizo katika eneo la chuo kiku anakosoma.

Kambakhsh anapinga vikali mashtaka hayo, akijitetea kwamba aliungama tu kufanya hivyo kutokana na kuteswa .

Hapo Januari 20,kijana huyu alihukumiwa kifo katika kesi ilioendeshwa faraghani bila hata kuruhusiwa wakili wa kumtetea.Kesi hiyo iliendeshwa huko Mahzar-e-Sharif.

Hukumu hiyo ikafutwa baadae na Mahkama ya rufaa.Hatahivyo, muandishi huyu itambidi kutumika kifungo cha miaka 20 korokoroni kwa hatia ambayo kwa muujibu wa kifungu cha 347 cha sheria za Afghanistan ,adhabu yake ya juu kabisa ni miaka 5 korokoroni.

Wakili anaemtetea Kambakhsh, Mohammad Afzal Nooristani, ameiambia Kamati yenye kuwatetea waandishi habari yenye makao makuu mjini New York (CPJ) kuwa mmoja kati ya mashahidi ,mwanafunzi mwezake katika darasa moja alieitwa tu Hamid aliambia Mahkama kwamba maafisa wa Usalama walimtembelea yeye siku chache baada ya kutiwa nguvuni mara ya kwanza mshtakiwa.Maafisa hao wa usalama wakamtishia kuwatia jamaa zake wote korokoroni ikiwa hatatoa taarifa juu ya madhambi anayotuhumiwa kufanya Kambakhsh.

Mwanafunzi huyo akawa shahidi mkubwa upande wa mashtaka .Yaqub Ibrahimi,ndugu wa mshtakiwa Kambakhsh, aliambia kamati inayowatetea waandishi habari jumaane wiki hii kuwa aliweza kuzungumza na nduguye sekunde chache tu baada ya kuhukumiwa. Akasema,

"Alistushwa sana,kwani akitaraji angeachwa huru hii leo ,lakini hukumu aliopitishiwa ni kali mno."

Serikali ya Afghanistan na wababe wa vita humo nchini , hawana sifa ya kuwanyonga waandishi habari,lakini ni maarufu kwa tabia yao ya kuwaandama waandishi habari ,kuwaweka kizuizini,kuwatendea maovu na kuwatisha-vikundi vinavyotetea haki za binadamu vinadai.

Serikali ya Rais Karzai nayo haikuonesha shauku kubwa ya kutetea uhuru wa kujieleza.Serikali ya Afghanistan ni dhamana ya alao visa 23 kati ya 45 vya kuwatisha-tisha waandishi habari,kuwaandama au kuwatia nguvuni kati ya mwezi Mei 2007 na Mei 2008.Na huo ni muongezeko wa 130% ukilinganisha na visa kama hivyo kipindi hicho hicho mwaka uliotangulia wa 2006.hii ni kwa muujibu wa kituo cha Nai Centre kinachotetea uhuru wa vyombo vya habari-Open Media.