1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yasema haitikiswi na vitisho vya Marekani

Saumu Mwasimba
11 Septemba 2018

Mahakama ya kimataifa ya uhaifu ICC imebainisha kuwa itaendelea na kazi zake bila ya kuogopa kufuatia vitisho vilivyotolewa na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton kwamba itawekewa vikwazo.

https://p.dw.com/p/34f6m
Niederlande Internationaler Gerichtshof (IGH) in Den Haag
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Corder

((Mahakama ya Kimataifa ya jinai mjini The Hague imesema itaendelea kuendesha shughuli zake bila ya kuvunjika moyo ikiwa ni siku moja baada ya mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton kutishia kuiwekea vikwazo mahakama hiyo,ikiwa itaanzisha uchunguzi wa shughuli za Marekani nchini Afghanistan.

Mahakama hiyo ya ICC imetowa taarifa ikisema kama mahakama ya sheria itaendelea kufanya kazi yake bila ya kuvunjika moyo,kwamujibu wa kanuni zake na muongozo wa utawala wa kisheria. Mahakama hiyo pia imesisitiza kwamba ni chombo huru na kisichokuwa na upendeleo na kinachoungwa mkono na nchi 123.

Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton ameupinga uhalali wa mahakama hiyo iliyoundwa mwaka 2002 kwa lengo la kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu wa kibinadamu sambamba na mauaji ya halaiki katika maeneo ambako wahusika huenda wakakwepa kuchukuliwa hatua za kisheria.

USA | Sicherheitsberater Bolton droht dem Internationalen Strafgerichtshof
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/A. Harnik

Hotuba ya Bolton ilitolewa jana ambapo ilikuwa ni siku ya mkesha wa kumbukumbu ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani,lakini pia hotuba hiyo imekuja katika wakati ambapo jaji wa ICC alikuwa akitarajiwa kutangaza uamuzi kuhusu ombi la waendesha mashtaka la kutaka kuanzisha rasmi uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Afghanistan na vikosi vya usalama vya Afghanistan,Taliban na wanamgambo wa mtandao wa Haqqami sambamba na vikosi vya Marekani na shirika la ujasusi na Afghanistan tangu May mwaka 2003. Madai dhidi ya wanajeshi wa Marekani yanahusisha vitendo vya utesaji na kuwafunga watu kinyume na sheria lakini katika hotuba yake Bolton aliishambulia ICC,katu Marekani haiwezi kushirikiana na chombo hicho ambacho kimeshakufa.

''Nataka kutowa ujumbe wa wazi na wa moja kwa moja kwa niaba ya rais wa Marekani. Marekani itatumia njia zozote inazoweza kuwalinda raia wetu na wale wa washirika wetu dhidi ya mashtaka yasiyokuwa ya haki ya mahakama hii isiyohalali. Hatutoshirikiana na Icc, Hatutotoa msaada kwa Icc na kwa uhakika hatutojiunga na Icc. Tutaiacha Icc iangamie yenyewe. Na hata hivyo kwa nia na malengo yote mahakama ya ICC kwetu sisi tayari imeshakufa.''

Israel Netanjahu empfängt US-Sicherheitsberater John Bolton
Picha: Getty Images/AFP/S. Scheiner

Bolton pia ameendelea kusisitiza kwamba Marekani siku zote itasimama na rafiki na mshirika wake Israel na kwamba kutokana na juhudi za Palestina za kujaribu kuchochea uchunguziwa ICC dhidi ya Israel wizara ya mambo ya nje ya Marekani itatangaza kuifunga ofisi ya chama cha PLO mjini Washington. Bolton ametanabahisha kwamba ikiwa wapalestina watakataa kuchukua hatua za kuanza mazungumzo ya moja kwamba na Israel,Marekani haitokuwa na haja ya kuachia shughuli za ofisi ya chama cha Palestina cha PLO.Vitisho vya Bolton juu ya Palestina vimejibiwa na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Palestina Saeb Erakat.

Utawala wa Trump unataka kuvuruga utaratibu wa sheria ya kimataifa kuhakikisha kwamba unabakia juu ya sheria na kukwepa kubeba dhamana.Ikiwa Marekani inaipinga kiasi hicho ICC kwanini ililiongoza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika kujaribu kumfikisha rais Omar al Bashir wa Sudan?Kwanini iliunga mkono kufunguliwa mashtaka viongozi wa Afrika katika mahakama ya ICC.

Kilichowekwa wazi pia katika hotuba ya Bolton ni kwamba utawala wa Trump utawapiga marufuku majaji wa ICC pamoja na waendesha mashtaka wa chombo hicho kuingia Marekani, pamoja na kuziwekea vizuizi fedha zao katika benki za nchi hiyo,na juu ya hilo kuwafungulia mashaka katika mahakama za uhalifu za Marekani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/REUTERS

Mhariri:Josephat Charo