1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaukosoa uamuzi wa Trump

Grace Kabogo
12 Juni 2020

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imemshutumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuidhinisha vikwazo dhidi ya maafisa wa ICC wanaowachunguza wanajeshi wa Marekani kwa madai ya uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3dfqk
Belgien Den Haag | Internationaler Strafgerichtshof
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Mahakama ya ICC imeviita vikwazo hivyo vya kiuchumi na usafiri ''visivyo vya kawaida'' na imeishutumu serikali ya Trump kwa kujaribu kuingilia utawala wa sheria na kesi za mahakama hiyo. ICC imesema hatua ya Marekani ni ya hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa mashambulizi ambayo hawakuyatarajia dhidi ya mahakama hiyo.

Agizo la Trump

Jana Trump alisaini agizo la utendaji litakalozidhibiti mali zilizoko Marekani za afisa yeyote wa mahakama ya ICC yenye makao yake makuu mjini The Hague, anayehusika na kuwachunguza au kuwashtaki wanajeshi wa Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema hawawezi kuzubaa wakiangalia tu watu wao wanatishwa na mahakama hiyo.

Pompeo ametoa ujumbe kwa washirika wake wa karibu duniani akisema wanaweza kuwa wanaofuata katika kuchunguzwa na ICC, na hasa nchi wanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO ambao wamekuwa wakipambana na ugaidi nchini Afghanistan pamoja na Marekani.

Donald Trump in Dallas
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP/A. Brandon

Wakati huo huo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch limesema utawala wa Trump unadhoofisha juhudi za ICC kupigania haki za waathirika waliofanyiwa uhalifu mkubwa.

Mkurugenzi wa sheria za kimataifa wa shirika hilo, Richard Dicker amesema vikwazo hivyo vinakiuka haki za binaadamu. Human Rights Watch imesema kwa kuilenga ICC, serikali ya Trump inaendelea kuwepo upande wa wale wanaofanya uhalifu na kuufunika na sio wale wanaowashitaki wahalifu.

Wasiwasi wa jumuia ya kimataifa

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu vikwazo hivyo. Msemaji wa umoja huo, Stephane Dujarric amesema wanauchukulia uamuzi huo kwa makini na wataendelea kufuatilia kwa karibu mambo yatakavyokwenda.

''Ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na ICC umeanzishwa kwa misingi ya makubaliano ya uhusiano, ambayo yaliidhinishwa na kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2004. Hivyo, tutaangalia athari zozote zinazoweza kujitokeza kwa kuzingatia utekelezaji wa makubaliano hayo,'' alisisitiza Dujarric.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell ameelezea ''wasiwasi mkubwa'' kuhusu hatua ya Marekani na amesema mahakama ya ICC inapaswa kuheshimiwa na kuungwa mkono na mataifa yote. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Stef Blok amesema anasikitishwa sana na uamuzi wa Marekani na kwamba Uholanzi inaiunga mkono Mahakama ya ICC iliyoko kwenye ardhi yake.

(AFP, DPA, AP, HRW https://bit.ly/37m28KV)