1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya kikosi cha UNAMID kupunguzwa Darfur

Saumu Mwasimba
14 Julai 2018

Baraza la usalama limeidhinisha kwa kauli moja azimio la kupunguzwa idadi kubwa ya wanajeshi wa UN na AU katika jimbo la Darfur Sudan.Ni kufuatia kupungua vita na kuimarika kwa hali jumla ya usalama katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/31RKw
UN Mission UNAMID
Picha: picture-alliance/dpa/A. G. Farran

Azimio hilo limepitishwa kwa kura zote 15 na inatarajiwa kwamba baadae pia  kikosi hicho cha UNAMID kitaondoka kabisa. Vita katika jimbo la Darfur vilianza mwaka 2003 Wasudan weusi walipoanzisha uasi wakiituhumu serikali ya Sudan inayohodhiwa na wenye asili ya kiarabu kwa ubaguzi. Serikali ya mjini Khartoum ilituhumiwa kulipiza kisasi kwa kutoa silaha kwa kundi la wapiganaji wa eneo hilo kutoka makabila ya wenye asili ya Kiarabu wanaohamahama na kuliachia kufanya ukatili dhidi ya raia,madai ambayo hata hivyo serikali hiyo ya Khartoum inayakanusha.

Kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kilianzishwa 2007 kikiwa na majukumu ya kusaidia kuwalinda raia wa jimbo hilo la Darfur. Katika kipindi cha miaka ya karibuni kufuatia mafanikio ya operesheni ya jeshi la serikali, uasi umepungua wa kikosi cha SLA kinachomuunga mkono mwasisi wake Abdul Wahid Elnur katika eneo la magharibi la Jebel Marra.

UN-Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Azimio la Umoja wa Mataifa linakaribisha hatua ya kuimarika hali ya usalama pamoja na kupungua kwa makabiliano ya kijeshi kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi ingawa Umoja huo bado una wasiwasi kwamba hali bado ni ya kuchukua tahadhari kufuatia shughuli za kuvunja usalama zinazofanywa na makundi yenye silaha pamoja na vikosi maalum vya serikali ya Sudan na makundi ya wanamgambo.

Chanzo cha migogoro

Wasser in Darfur
Picha: UN

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linasema kwamba migogoro ya jamii mbali mbali kuhusina na ardhi, maji na rasilimali nyinginezo, uhamiaji na ukabila ni masuala ambayo yamepungua kwa kiasi kikubwa ingawa bado ndio chachu kubwa ya kuzuka migogoro na vurugu katika jimbo hilo la Darfur.

Mkuu wa shughuli za kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Jean Lacroix ameliambia baraza la usalama mwezi uliopita kwamba hali ya Darufr imebadilika kwa kiwango kikubwa na kuonesha kuimarika na kwamba Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika umependekeza kupunguza idadi kubwa ya wanajeshi wake.

Juni 2016 kikosi cha UNAMID kilikuwa na wanajeshi jumla ya 15,845 na polisi 3,403,idadi hiyo ilipinguzwa kwa kiwango kikubwa kufikia mwishoni mwa mwezi Januari. Tathmini ya mkakati wa UN na AU  karibuni ikapendekeza kupunguzwa zaidi idadi iliyobakia ya wanajeshi 8,735 hadi 4,050 huku idadi ya polisi 2,500 ikitakiwa kupunguzwa hadi 1,870. Azimio hilo lililoidhinishwa Ijumaa usiku litaanza kutekelezwa katika kipindi cha siku 90.

Mwandishi: Yusuf Saumu

Mhariri: Jacob Safari