1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliokufa kutokana na moto yafikia 40, Urusi

3 Agosti 2010

Rais Medvedev ametangaza hali ya hatari kutokana na janga la moto.

https://p.dw.com/p/Oanb
Takriban eka 300,000 inawaka moto nchini Urusi.Picha: AP

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev ametangaza hali ya hatari katika maeneo ya Mairi El, Mordovia, Vladimir, Voronezh, Nizhny Novgorod na Ryazan. Kutokana na taarifa iliyotumwa kwenye tovuti ya ikulu ya Urusi, Kremlin, amri hiyo itawaruhusu maafisa wawazuie raia kuelekea katika maeneo ambayo ni hatari kwa maisha yao na wanajeshi waweze kuudhibiti moto huo.

Katika hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni nchini humo, Rais Medvedev alisema ulegevu wowote unaweza kusababisha janga lisiloweza kuzuiwa na kwamba jukumu kubwa la serikali ni kuwasaidia wahanga warejee katika maisha yao ya kawaida.

Waziri mkuu wa Urusi, Vladimir Putin amesema kuna uwezekano wa kuomba msaada wa wasamaria wema wawasaidie maafisa wanaojitahidi kuuzima moto huo.

Wizara ya afya jana ilisema idadi wa waliofariki imefikia 40 na eneo lililoathirika zaidi ni la Ninhny Novgorod ambapo watu 19 wamekufa. Kiongozi wa kanisa la Kiothodoksi nchini humo aliongoza misa katika eneo hilo na waumini waliomba ili mvua inyeshe.

Wizara ya maendeleo imesema kiasi ya nyumba 1,875 zimeteketezwa na moto huo ambao umewaacha zaidi ya watu 2000 bila makaazi na takriban eka laki tatu ya ardhi inawaka moto.

Waldbrände in Russland
Nyumba 1,875 zimeteketezwa, zaidi ya wakaazi 2,000 wameachwa bila makaazi.Picha: AP

Waziri wa masuala ya dharura, Sergei Shoigu amesema kwamba jana pekee moto huo ulienea haraka kutokana na upepo mkali katika eneo la Lipetsk na kuziteketeza nyumba 50 . Kijiji kizima cha watu 155,000 kiliteketezwa katika janga hilo la moto lilotajwa na rais Medvedev kama janga kubwa kuwahi kushuhudiwa kwa kizazi.

Mji mkuu wa Urusi, Moscow jana ulikuwa na ukungu uliosababishwa na moshi wa moto unaowaka mikoani na leo asubuhi kulikuwa na harufu kali ya moshi.

Waziri mkuu, Vladimir Putin ambaye aliongoza kundi la waokoaji katika maeneo yaliyoathirika zaidi alitoa maagizo makali kwa maafisa husika katika mkutano na magavana wa maeneo yanayozongwa na moto.

Alisema anataka kuona mipango madhubuti ya ujenzi upya katika kila mkoa, kila wilaya na kila nyumba na pia apewe majina ya wale wote walioathirika. Waziri mkuu huyo ambaye mara nyingi huwa hakosolewi alijikuta akishambuliwa na walioathirika na janga hilo ambao walionekana kuwa na hasira.

Wataalamu wa utabiri wa hali ya hewa wameonya kwamba hakuna matumaini ya viwango vya joto kupungua nchini humo na vipimo vya kati ya nyusi 35 na 42 vinatarajiwa mjini Moscow na maeneo ya kati ya Urusi mnamo siku zijazo.

Mwandishi, Peter Moss /AFP/AP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed