1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wanawake yaongezeka magerezani Afrika Mashariki

19 Oktoba 2023

Washiriki katika Kongamano la Mashariki mwa Afrika kuhusiana na haki za wanawake katika jinai lililofanyika nchini Uganda wameelezea wasiwasi wao kuhusu kasi ya ongezeko la wanawake wafungwa magerezani na pia korokoroni.

https://p.dw.com/p/4XlSW
Paraguay I Aufstände im Tacumbu Gefängnis beendet
Picha: Jorge Saenz/AP/picture alliance

Ili kukabiliana na hali hiyo kwa kuzingatia jinsia na majukumu ya wanawake katika jamii, wadau kutoka mataifa hayo wanakutana mjini Kampala kubuni na kuwasilisha mapendekezo kwa nchi za Afrika kuchunguza upya jinsi kesi na hukumu kwa wanawake zinavyotakiwa kutilia maanani maslahi yao. 

Roselyn Kodet ni mwathirika wa haki ya jinai. Mahakama haikuzingatia chanzo cha yeye kutenda mauaji bila kukusudia.

Wanawaeke wa Senegal na haki ya kumiliki ardhi

Alihukumiwa miaka saba akiwaacha ndugu zake aliokuwa akiwatunza ambao pia ni mayatima pamoja na wanawe baada ya mumewe kuugua ugonjwa wa akili.

Ni katika hali hii ndipo Grace Dafa kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria  kutoka Tanzania anasema ni "muhimu wa kuwachukulia wanawake wafungwa na pia wale wanaokutwa wamevunja sheria kuwa kundi ambalo linahitaji kuchunguzwa kilichowasababisha kushiriki vitendo vya jinai."

Hali ya magereza Uganda

Kulingana na Kamishna Mkuu wa Magereza ya Uganda, Johnson Byabashaija, kesi dhidi ya theluthi moja ya wanawake wafungwa katika magereza ya Uganda ni kuhusiana na mauaji.

"Jamii ichunguze na kushughulikia vyanzo vya hali hiyo. Sisi kama magereza hutatizika sana kuwashughulikia wanawake wafungwa kwa sababu wana mahitaji maalum kutokana na jinsia yao pamoja na majukumu ya kuwalea watoto." Anasema mkuu huyo wa magereza.

Mwanaharakati wa Iran Narges ashinda tuzo ya Nobel 2023

Wadau kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Rwanda na Kenya walikuwa wanakutana kubadilishana uzoefu na mikakati ya kuwasaidia wanawake wanaokabiliwa na mashtaka ya jinai kurejelea maisha ya kawaida.

Makosa ya kizamani

Kinachowakera ni kwamba baadhi ya sheria wanazoelezewa kukiuka wanawake  ni za kikoloni na hazina nafasi katika maisha ya sasa. Miongoni mwa hizo ni kushiriki biashara ya pombe za kienyeji, kuzurura, kusababisha bughdha kwa umma na kadhalika.

Kongamano hilo lilifadhiliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia kukabiliana na matumizi ya mihadharati, ufisadi na pia uhalifu (UNODC) kwa ushirikiano na kituo cha kimataifa cha kurekebisha sheria za jinai (PRI).

Mapendekezo kutoka mkutano huo yalitarajiwa kuwasilishwa kwa Umoja wa Afrika ili kutoa hamasa kwa mataifa ya Afrika kuchunguza upya sera na sheria kuhusiana na mfumo wa kisheria kwa wanawake.

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala