1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IOC yatangaza mkakati dhidi ya rushwa

12 Desemba 2015

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki inataka kuhakikisha kuwa mabilioni ya dola ya fedha zinazopewa washika dau kwa ajili ya maendeleo ya michezo yanatumika ipasavyo na itataka ripoti za hesabu kwa kila mchango unaotolewa

https://p.dw.com/p/1HM6n
Thomas Bach Präsident Internationales Olympisches Komitee
Picha: picture-alliance/dpa/L. Gillieron

Hayo yamesemwa na Rais wa IOC Thomas Bach mwishoni mwa mkutano wa Bodi ya Utendaji ya IOC mjini Lausanne, Uswisi. Amesema "Tunataka kuzuia, au tunachotaka kutimiza - ni vyema niseme hivi – ni kuwa fedha hizi, ambazo zinatokana na michezo zinaenda kwa michezo na maamuzi – ya zinazomnufaisha, mwishowe, kutoka kwa michango hii – maamuzi haya yanachukuliwa kwa kuheshimu sheria za uongozi bora".

IOC, ambayo ina wasiwasi kuhusiana na kashfa zinazoendelea kuliandamana Shirikisho la Kandanda la Kimataifa – FIFA na lile la Michezo – IAAF, ina hamu ya kuhakikisha kuwa malipo muhimu yanayopewa mashiriksiho ya michezo ya kimataifa , Kamati za Kitaifa za Olimpiki – NOC, na kamati za maandalizi yanatumiwa kwa uwazi na uwajibikaji.

Aidha Bach aliangazia masuala mengi yanayoathiri matayarisho ya Mashindano ya Olimpiki ya 2016 mjini Rio de Janeiro, ikiwemo wasiwasi kuhusiana na kuporomoka uchumi wa Brazil, madai ya rushwa, wasiwasi kuhusu ubora wa maji na uwezekano wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff. Licha wasiwasi huo, rais huyo wa IOC ana matumaini kuwa michezo hiyo itakuwa ya kufana

Bach aliongeza kuwa IOC inashikiriana na Mashirika ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za kuongeza misuli nguvu ili kuhakikisha kuwa wanamichezo safi nchini Kenya na Urusi wanaendelea kufanyiwa vipimo vya nje ya mashindano wakati mashirikisho yao yakiendelea kuchunguzwa. "IOC, kwa upande wake – kama unavyoona kutoka kwa azimio hili – tumewasiliana na washirika wetu na Mashirika ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kuongeza Misuli Nguvu – NADO ili kuhakikisha kuwa nchi hizi mbili – Urusi na Kenya ambako vipimo vya nje ya mashindano havifanyi kazi kwa sasa kwa sababu shirika la NADO nchini Kenya halifanyi kazi kikamilifu na lile la Urusi limesimamishwa, kwamba wakati wa kipindi hiki wanamichezo kutoka michezo yote wanajiunga na mpango mzuri wa vipimo vya nje ya mashindano ili kuwalinda wanamichezo safi".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Sessanga