1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran: Marekani ioneshe nia kufufuliwa mkataba wa nyuklia

20 Septemba 2023

Rais wa Iran Ebhahim Raisi ameihimiza Marekani kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kutaka kuufufua mkataba wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu ambao Washington ilijondoa mwaka 2018.

https://p.dw.com/p/4WZxG
Rais Ebrahim Raisi wa Iran
Rais Ebrahim Raisi wa Iran akihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa Picha: Seth Wenig/AP/dpa/picture alliance

Akihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kiongozi huyo wa Iran amesema uamuzi wa Marekani wa kujitoa kwenye mkataba huo ulikuwa ni ukiukaji wa makubaliano yenyewe na Washington inafaa kuonesha nia ya uhakika wakati inapigia debe kufufuliwa kwa utekelezaji wake.

Rais Joe Biden wa Marekani alijaribu kuanzisha mashauriano ya kuufufua mkataba huo muda mfupi baada ya kuingia madarakani lakini juhudi hizo zimesimama kwa karibu mwaka mmoja baada ya Iran kukataa mapendekezo ya wapatanishi wa Umoja wa Ulaya. 

Wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wanaamini siyo rahisi tena kuufufua mkataba huo wa mwaka 2015, kwa sababu Iran imekiuka masharti mengi ikiwa ni pamoja na kuongeza urutubishaji wa madini ya Urani kwa ajili ya mradi wake wa nyuklia.