Iran yaishutumu Marekani kwa "Uraibu wa kupindukia na Iran"
17 Februari 2019Hii "inasikitisha, lakini wakati huo huo ni hatari sana," Zarif alisema katika mkutano wa usalama mjini Munich, ambako alilaani kile alichokieleza kuwa ni "hotuba za kijinga za chuki zinazotolewa na maafisa wa Marekani."
Pence alisema jana Jumamosi (16.02.2019) kwamba Iran inatafuta uwezo wa kutekeleza "mauaji mengine ya Wayahudi ya Holocaust" na kutoa wito kwa washirika wa Marekani katika bara la Ulaya kufuata kujitoa kwa Marekani katika makubaliano ya kinyuklia na Iran ya mwaka 2015.
Iran inaishutumu Iran kwa kuingilia katika mizozo katika eneo hilo na imejitoa binafsi kutoka katika makubaliano ya kinyuklia na nchi hiyo mwaka jana, na kuiweka Iran katika mzozo wa kiuchumi wakati rais Donald Trump alipoanzisha upya vikwazo dhidi ya taifa hilo linalosafirisha mafuta.
Benjamin Gantz, mnadhimu mkuu wa zamani wa jeshi la Israel, amewataka wajumbe waliokuwapo katika mkutano huo wa Munich "kutoa amini maneno yake matamu" wakati wa hotuba ya kumjibu Zarif. "msipumbazwe na uongo wake," alisema.
"Kama mnadhimu mkuu wa zamani wa jeshi la Israel , niliona taarifa za uhakika mimi binafsi kuhusiana na kile kinachotokea nchini Iran," Gantz alisema. "Kwa hiyo , naweza kuwaambia kwa uhakika zaidi kwamba utawala ambao Bwana Zarif anauwakilisha ni utawala wa uovu."
Hasimu mwingine wa Iran hakuwakilishwa katika mkutano huo baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia Adel al-Jubair kufuta uwakilishi wake katika mkutano huo.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, naibu waziri mkuu wa Qatar na waziri wa mambo ya kigeni, alitumia mkutano huo kuonya dhidi ya hali inayoongezeka ya mgawanyiko katika mashariki ya kati.
"Tunashuhudia ongezeko katika eneo hili mgawanyiko na kwamba hali hiyo inaongezeka siku hadi siku," amesema.
Juni mwaka 2017 , Saudi Arabia, Umoja wa Falme za kiarabu, Bahrain na Misri zilivunja uhusiano wa kibalozi na kibiashara na Qatar, zikiishutumu kwa kuunga mkono ugaidi, madai ambayo Qatar inayakana.
Wakati huo huo Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran amesema leo kwamba Mataifa ya Ulaya yanapaswa kufanya juhudi zaidi badala ya kusema tu iwapo yanataka kulinda makubaliano yenye lengo la kuidhibiti Iran kutopata silaha za kinyuklia baada ya kujitoa kwa Marekani, na kuishutumu nchi hiyo kuwa ndio "chanzo kikuu kwa eneo la mashariki ya kati kutokuwa na uthabiti".
Mohammad Javad Zarif amesema mjini Munich kwamba mfumo wa kubadilishana bidhaa unaofahamika kama INSTEX , ambao umetayarishwa na Ufaransa, Ujerumani na Uingereza mwezi uliopita kuruhusu biashara kuendelea katika ya Iran na mataifa hayo ili kuepuka vikwazo vya moja kwa moja vya kifedha, na kuepuka uwezekano wa kuwekewa vikwazo na Marekani hautoshi.
Amesema kwamba Ulaya inapaswa kuwa tayari kulowa iwapo inataka kuogelea dhidi ya wimbi hatari la kujitoa kwa Marekani katika makubaliano ya kinyuklia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Zainab Aziz