1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yashambulia vituo vya jeshi la Marekani Iraq

Iddi Ssessanga
8 Januari 2020

Iran imeshambulia vituo vya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq mapema Jumatano, kulipa kisasi cha mauaji ya kamanda wake ambaye kuuawa kwake wiki iliyopita kumechochea wasiwasi wa kuzuka upya kwa vita Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/3VsZW
Iran Ajatollah Ali Chamenei bei einer Kundgebung in Teheran
Picha: Reuters/Official Khamenei website

Kiongozi wa juu wa Iran Ali Khamenei amesema mashambulizi hayo ya makombora yalikuwa kibao cha usoni kwa Marekani na kwamba wanajeshi wa Marekani wanapaswa kuondoka katika kanda hiyo. Alikuwa anahutubia mkusanyiko wa Wairan waliokuwa wanaimba "kifo kwa Marekani".

Televisheni ya Taifa ya Iran ilisema Iran ilifyatua makombora 15 kuelekea maeneo ya Marekani. Jeshi la Marekani lilisema maeneo yasiopungua mawili yanayohifadhi wanajeshi wa vikosi vya muungano nchini Iraq yalilengwa majira ya saa saba na nusu usiku. Iraq imesema makombora 22 yalifyatuliwa.

Maafisa wa Iran wamesema Tehran haikutaka vita na mashambulizi yake yamehitimisha majibu yake kwa mauaji ya Qassem siku ya Ijumaa, jenerali ambaye mazishi yake baada ya siku kadhaa za maombolezi yalifanyika wakati makombora hayo yalipofyatuliwa. Televisheni ya Iran iliwaonesha waombolezaji wakishangilia.

Iran Feier nach Raketenangriff auf US-Militärbasen im Irak
Waombolezaji wakishangilia baada ya Iran kufyarua makombora kuelekea vituo vya jeshi la Marekani nchini Iraq.Picha: Reuters/WANA/N. Tabatabaee

Tathmini ya maafa na uharibifu yafanyika

Rais wa Marekani Donald Trump amesema tathmini inaendelea kufanyika kuhusu idadi ya waliouawa katika mashambulizi hayo pamoja na kiwango cha uharibifu na kwamba angetoa tamko siku ya Jumatano, lakini akaongoeza katika ujumbe wake wa Twitter kwamba kila kitu kiko sawa, na kwamba Desemba 2018 alitembelea kituo cha jeshi la anga cha Ain al-Asad, mojawapo ya vilivyolengwa katika mashambulizi ya Iran.

Chanzo kimoja kimesema mapema kwamba ishara za mwanzo zinaonesha hakukuwa na maafa yoyote kwa upande wa Marekani, huku maafisa wengine wa Marekani wakikataa kuzungumzia suala hilo. Televisheni ya taifa ya Iran ilisema "magaidi 80" wa Marekani waliuawa na kwamba helikopta za Marekani na vifa vya kijeshi viliharibiwa, bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote wa namna walivyopata taarifa hizo.

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema matumizi ya silaha yanapaswa kusimama. Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana Ijumaa wiki hii kujadili nini kanda hiyo inaweza kufanya kuhusu mzozo huo.

Kassem Soleimani, der Kommandeur der iranischen Al-Kuds-Brigaden
Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Qudsi alieuwa na Marekani na kuzusha tafrani nchini Iran.Picha: picture-alliance/dpa/AP/E. Noroozi

"Sote tuna jukumu la kufanya kila linalowezekana kufufua mazungumzo bila kuchoka. Umoja wa Ulaya una mengi ya kufanya kwa namna yake. Tumeanzisha uhusiano wa muda mrefu na wadau wengi katika kanda na zaidi ili kutuliza hali," alisema von der Leyen.

Ujerumani, Uingereza, Umoja na mataifa mengine yamekosoa mashambulizi hayo huku mengine yakitangaza kupunguza vikosi vyao vilivyopo nchini Iraq. Ufaransa kwa upande wake imesema haina mpango wa kuondoa wanajeshi wake. Iran imetishia kulenga miji ya Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Haifa nchini Israel iwapo Marekani itajibu mashambulizi ya Jumatano.

Vyanzo: Mashirika