1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yashiriki mkutano wa kilele Vienna

30 Oktoba 2015

Mataifa yenye nguvu duniani, zikiwamo nchi hasimu Iran na Saudi Arabia, kwa mara ya kwanza yanakutana kwa mazungumzo leo hii mjini Vienna wakiwa wanatafuta suluhisho la vita vya Syria.

https://p.dw.com/p/1Gwwt
Wien: Vortreffen zur Syrien-Konferenz in Wien - John Kerry und Javad Sarif
Waziri wa mmabo ya nje wa Marekani, John Kerry, akiwa na mwenziwe wa Iran, Javad Zarif.Picha: picture-alliance/dpa

Wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali wamekusanyika mjini Vienna kujadili hatima ya Rais wa Syria Bashar al-Asaad, ambaye amekaidi wito wa nchi za magharibi zilizomtaka ajiuzulu.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema kuwa nchi mbalimbali kuweza kukubali kukutana kwa mazungumzo tayari hiyo ni hatua muhimu katika mchakato wa kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria.

"Ninaamini kitendo cha pande zote kukubali kukutana tayari ni mwanzo mzuri, kitu ambacho wiki moja nyuma ilikuwa tabu kufikiria kinawezekana," alisema Federica Mogherini.

Hata hivyo, hakujakuwa na dalili yoyote inayoonesha kuwepo kwa wawakilishi wa serikali ya Syria au upinzani katika mazungumzo hayo yanayolenga kusitisha vita vya miaka minne sasa.

Österreich vor Syrien-Konferenz in Wien Federica Mogherini
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: picture-alliance/H. Punz

Iran yashiriki kwa mara ya kwanza

Kama ishara ya kukua kwa ushawishi wake wa kidiplomasia, Iran mfadhili wa muda mrefu wa utawala wa Asaad, kwa mara ya kwanza itahudhuria mazungumzo hayo, miezi michache baada ya kukamilisha makubaliano ya kudumu kuhusu mpango wake wa nyuklia na mataifa yenye nguvu duniani.

Afisa muandamizi kutoka Mashariki ya kati na mwenye ufahamu wa msimamo wa Iran ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, jana usiku kabla ya mazungumzo ya leo, Iran iliashiria kuwa pengine itabadilisha msimamo wake wa kumtaka Assad kubaki madarakani.

Iran imesema inaweza ikakubali kuwepo kipindi cha mpito cha miezi sita na baada ya hapo hatima ya Assad itaamuliwa kwa uchaguzi mkuu.

Wakati wote huu vita vikiwa vinaendelea na kusababisha vifo vya watu 250,000 na wengine milioni 10 kupoteza makaazi yao, mshirika mkuu wa Asaad, Iran haikualikwa kuhudhuria mikutano ya kimataifa ya kuitafutia amani Syria, mikutano ambayo yote ilimalizika bila ya kupatikana suluhisho.

Majadiliano ya leo yatakuwa ni ya kwanza kuishirikisha Iran.

Marekani imesema inasubiri kusikia kauli za Iran na mshirika mwingine wa Asaad, Urusi, kama zitakuwa tayari kuachana na kiongozi huyo wa Syria, ambaye Marekani, nchi kadhaa za Ulaya pamoja na washirika wao wa nchi za kiarabu ndiye wanayemlaumu kwa umwagikaji wa damu nchini humo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afpe

Mhariri: Josephat Charo