1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasisitiza itaendelea kutengeza makombora

Caro Robi
29 Januari 2019

Iran imepuuza mbali wito kutoka kwa Marekani na Umoja wa Ulaya kusitisha mpango wake wa kutengeza makombora lakini nchi hiyo imesema haina mipango ya kuongeza uwezo wake wa kutengeza makombora ya masafa marefu.

https://p.dw.com/p/3CM8M
Iran Ballistische Rakete
Picha: Getty Images/F.Bahrami

Waziri wa ulinzi wa Iran Amir Hatami amenukuliwa na shirika la habari la Tasnim akisema maadui wanataka nguvu za Iran za kutengeza silaha kuvunjwa lakini mara kwa mara wamesema uwezo wao wa kutengeza makombora sio suala la kujadiliwa.

Katibu wa baraza la usalama wa kitaifa wa Iran pia amesema nchi yake itaendelea kuufanyia kazi mpango wake wa kuunda makombora.

Ali Shamkhani ambaye ni mshirika wa karibu wa kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema nchi hiyo haina vikwazo vya kisayansi wala kiufundi kuongeza nguvu zake za kijeshi, lakini kulingana na juhudi zake za kuendelea kujihami inaendelea kuboresha uwezo wake wa kutengeza makombora lakini haina nia ya kuongeza urefu wake.

Jumuiya ya Kimataifa ina wasiwasi

Rais wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake kutoka kwa makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa kinyukulia wa Iran na kuirejeshea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi kwa hoja kuwa makubaliano hayo kati ya nchi zenye nguvu zaidi duniani na Iran hayakushughulikia suala la uwezo wa Iran kutengeza makombora na ushawishi wake katika masuala ya kanda ya Mashariki ya Kati.

Iran Hassan Rohani
Rais wa Iran Hassan RouhaniPicha: Getty Images/AFP

Wiki iliyopita, Ufaransa ambayo bado inayaunga mkono makubaliano hayo ya kudhibiti mpango wa kinyuklia wa Iran yaliyofikiwa mwaka 2015, ilisema iko tayari kuiwekea nchi hiyo vikwazo zaidi iwapo hakutapigwa hatua katika mazungumzo kuhusu mpango wake wa kutengeza silaha za kinyuklia.

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoambatana na makubaliano ya kinyuklia kuhusu Iran ya 2015 yaliitaka nchi hiyo kujizuia kwa hadi miaka minane dhidi ya kutengeza makombora yanayoundwa kwa ajili ya kurusha silaha za kinyuklia.

Lakini Iran imesema haikiuki azimio hilo na imekanusha kuwa makombora yake yana uwezo wa kubeba silaha za kinyuklia. Marekani pia imeitaka Iran kukomesha teknolojia yake ya kuzindua satilaiti, ikisema ina wasiwasi kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kutumika kurusha kombora lenye bomu lenye baruti.

Iran imesema itaendelea kuboresha teknolojia yake ya urushaji wa makombora ili kuimarisha maisha ya watu wake na kuongeza nguvu zake kitekonolojia. Jaribio la nchi hiyo kutuma satilaiti kwenda mzingo wa dunia ulifeli mwezi huu kwani roketi yake haikuwa na kasi ya kutosha katika hatua ya tatu.

Mwandishi; Caro Robi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga